Na Zahoro Mlanzi
SEKRETARIETI ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limemshtaki kwa mara nyingine Ofisa Habari wa Klabu ya Yanga, Louis Sendeu, kwa
Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya shirikisho hilo,
kutokana na kumtolea maneno makali mwamuzi Alex Magahi wa Mwanza.
Sendeu mara baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya Yanga na Ruvu Shooting uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, alidai kwamba, mwamuzi huyo alishindwa kutafsiri sheria 17 za soka na ndio maana, wanawekewa mazingira magumu ili Yanga isifanye vizuri na kuweka upenzi kwa timu anayoishabikia (Simba), iendelee kusonga mbele.
Hatua hiyo ya Sendeu ilitokana na mwamuzi huyo kumwonesha kadi ya pili ya njano ikafuatia nyekundu, Haruna Niyonzima 'Fabregas', kutokana na kujiangusha ndani ya eneo la hatari, kitendo ambacho Yanga inadai hakupaswa kupewa adhabu hiyo, badala yake ingekuwa penalti.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura, alisema Sendeu alimtolea maneno makali mwamuzi huyo, huku akijua alitakiwa kufanya nini, baada ya kuona haki haikutendeka kwa timu yake.
"Maneno yale aliyoyatoa, akidai mwamuzi ni mwanachama wa Simba, anaisaidia Simba ili izidi kusonga mbele, hakupaswa kuzungumza vile kwani inamhatarishia usalama wake, ilipaswa afuate taratibu zinazotakiwa, hivyo sekretarieti imeamua kumshtaki kwa kamati ya nidhamu,“ alisema Wambura.
Alisema kauli hiyo inamtengenezea chuki mwamuzi huyo, katika maisha yake ya kila siku kwa tuhuma alizotoa Sendeu kwamba, kadi aliyopewa Fabregas haikuwa halali, angepeleka malalamiko yao kwa kamati husika.
Alisema kwa sasa wanasubiri kamati hiyo ipange tarehe ya kukutana kusikiliza mashtaka hayo pamoja na yale ya kwanza ambayo yanamhusu Sendeu na Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage, ambao kwa nyakati tofauti waliyumbisha mchezo wa Ngao ya Jamii.
Sendeu kwani amesoma shule gani?,Kama amekwenda shule basi nafikiri alikuwa anahudhuria darasani tu lakini hakuna alichopata kutoka shule.Hivi mchezaji akijiangusa makusudi kwenye penalti box anatakiwa apewe adhabu gani?.Sasa nafikiri anatakiwa apewe filimbi ili achezeshe mpira badala ya kutowa visingizio visivyo kuwa na kichwa wala miguu.Kwanza sijui kama alishawahi kucheza huo mpira.Hivi timu gani alikuwa anachezea katika ujana wake.
ReplyDelete