14 September 2011

Simba, Polisi ni vita

Na Zahoro Mlanzi

VINARA wa Ligi Kuu Bara, timu ya Simba, leo itajitupa uwanjani kusaka pointi tatu dhidi ya Polisi Dodoma, katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.Simba
itashuka kwenye Uwanja wa Azam Chamazi kwa mara ya kwanza, tangu ujengwe.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii, watakuwa wakihitaji ushindi katika mchezo huo ili wazidi kuchanja mbuga katika ligi hiyo inayoonekana kuwa na ushindani mkubwa msimu huu, kutokana na kutokuwa na matokeo ya kutabirika.

Wakati Simba ikiwaza hivyo, Polisi Dodoma nayo itakuwa na ndoto za kupata ushindi wa kwanza tangu kuanza kwa ligi hiyo, na pia kuvunja rekodi ya Simba ya kutofungwa na timu yoyote mpaka sasa.

Vinara hao wanaongoza ligi wakiwa na pointi 10,  kwa kushinda michezo mitatu dhidi ya Coasta Union ya Tanga bao 1-0, JKT Oljoro ya Arusha mabao 2-0 na Villa Squad bao 1-0 na kutoka suluhu na Azam FC, na nyavu kushindwa kutikiswa mpaka sasa.

Timu hiyo inayofundishwa na Kocha Mkuu, Moses Basena,  ambapo aliuzungumzia mchezo huo kwa kusema kuwa, hakuna timu dhaifu katika ligi hiyo, watahakikisha wanaibuka na ushindi ili kuzidi kukaa pazuri katika msimamo wa ligi hiyo.

"Maandalizi yanaendelea vizuri na kama unavyojua, matokeo yetu ya mchezo wa mwisho tumetoka suluhu na Azam, ni matokeo mazuri ambayo yanatufanya kuangalia wapi tulipokosea ili katika michezo inayofuata,  hususan wa kesho (leo), tunafanya vizuri zaidi," alisema Basena.

Katika safu ya ushambuliaji, timu hiyo itaongozwa na Gervais Kago na Haruna Moshi 'Boban',  ambao inaonekana kadri wanavyocheza pamoja, ndivyo wanavyozidi kuelewana, sawa na mabeki Juma Nyosso na Victor Costa 'Nyumba'.

Kwa upande wa Polisi, yenyewe itaongozwa na Kulwa Mobby, Hamad Kambangwa na Bryton Mponzi, ambao tayari kila mmoja amecheka na nyavu mara moja moja, hivyo mabeki wa Simba watakuwa na kazi ya ziada kuhakikisha washambuliaji hao hawatikisi nyavu zao.

Katika msimamo wa ligi hiyo, Polisi ipo katika nafasi ya 12, ikiwa imecheza michezo minne,  ikitoa sare mitatu na kufungwa mmoja na kujikusanyia pointi tatu.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwenye uwanja huohuo, kwa African Lyon kuikaribisha Yanga, mchezo ambao utakuwa na ushindani mkubwa kutokana na matokeo ya timu hizo.

No comments:

Post a Comment