14 September 2011

Taasisi ya tiba asili yadaiwa kukwamisha utafiti wa dawa

Na Flora Amon

CHAMA cha Tiba Asilia nchini (ATME), kimesema Taasisi ya Tiba Asili iliyopo Chini ya Chuo Kikuu cha Tiba ya Sayansi na Afya za Jamii Muhimbili (MUHAS), kimeshindwa
kumaliza utafiti wa dawa ya miti shamba ambayo utafiti wa awali umebaini uwezo wa dawa hiyo kupunguza makali ya virusi vya ugonjwa wa UKIMWI.

Kukwama kwa utafiti huo, kumetokana na ukosefu wa fedha za kumalizia utafiti tangu mwaka 2003.

Akizungumza Dar es Salaam jana katika kilele cha Siku ya Tiba Asili kwa Mwafrika, Katibu Mkuu wa ATME, Bw. Athumani Peleu, alisema hadi sasa utafiti wa dawa hiyo haujakamilika ili jamii kubwa iweze kunufaika na matibabu yake.

“Dawa hii tuliifanyia utafiti wa awali baada ya kupata fedha kutoka Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Taasisi ya Tiba Asili imeshindwa kumalizia utafiti baada ya kukosa fedha,” alisema Bw. Peleu.

Alisema kwa kutambua umuhimu na uwezo wa dawa hiyo katika kupunguza makali ya VVU, wanamuomba Rais Jakaya Kikwete asaidie kufanikisha utafiti huo ili ianze kutumika.

“Yawezekana Rais Kikwete hajui kama kuna dawa ya asili ambayo ina uwezo mkubwa wa kupunguza makali ya VVU lakini utafiti wake umekwama, tunamuomba atusaidie katika hili ili iweze kutumika,” alisema.

Aliongeza kuwa kama utafiti wa dawa hiyo utamalizika haraka na kuanza kutumika, jamii kubwa inayokabiliwa na ugonjwa huo itanufaika pamoja na kuuzwa nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment