Na Godfrey Ismaely
MAKAMU wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal, amesema anashawishika kuviagiza vyuo vikuu mbalimbali nchini hasa vinavyoandaa walimu wa sayansi, kudaili wanafunzi wengi
wa kike ili kupunguza tatizo la wanaume kukwepa fani.
Dkt. Bilal aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akifungua jengo la mihadhara, katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), ambapo uzinduzi huo, ulikwenda sambamba na harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa jengo la maabara.
“Kutokana na uzoefu nilionao, nashawishika kuviagiza vyuo vikuu kama DUCE na vingine kuangalia namna ya kutoa kipaumbele kwa wanafunzi wa kike wanaosoma masomo ya sayansi ili waweze kufundisha katika shule zetu zikiwemo za kata,” alisema.
Alisema nchini Tanzania, asilimia kubwa ya wanafunzi wanaodailiwa katika vyuo vikuu ili kusomea masomo ya sayansi, wanafanya kazi hiyo kwa muda wanaotaka kuliko wanawake.
Aliongeza kuwa, wanawake ni wavumilivu hivyo siyo vibaya kama jitihada za kuwawezesha katika masomo ya sayansi zikafanyika kwani wanaume hufanya kazi ya kufundisha kwa muda mfupi na kuhama fani wakidai wanaenda kutafuta maslahi zaidi hivyo Serikali kujikuta ikipata hasara.
Dkt. Bilal alikitaka chuo hicho, kuhakikisha kinazalisha walimu wa kutosha ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu nchini na kuwafanya Watanzania wote kupata elimu bora.
“Najua tatizo la kupatikana walimu katika ngazi ya vyuo vikuu, linaanzia ngazi ya chini, nawaomba tusifanye hali hii kuwa kigezo cha kushindwa kuongeza idadi ya walimu wa sayansi, tuliweza tukafanikiwa hivyo mkianza tutafanikiwa,” alisema Dkt. Bilal.
Alisema ujenzi wa jengo hilo lenye kumbi tatu ambalo lina uwezo wa kuingiza wanafunzi 2,000 kwa wakati mmoja, umetokana na fedha za Serikali ambazo zilitolewa mwaka 2007 ili kuwawezesha wanafunzi kupata mazingira bora ya kusomea.
Katika hatua nyingine, Dkt. Bilal aliwaongoza watumishi wa chuo hicho, wanafunzi na wageni mbalimbali, kusimama kwa dakika moja ili kuwaombea Watanzania ambao walipoteza maisha katika ajali ya meli visiwani humo.
Alisema Serikali ya Muungano ambayo inaongozwa na Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein, waliweza kuonesha umoja wao katika kuhakikisha wafiwa wanapata msaada wa Serikali.
“Ajali hii ambayo imehusisha meli ya Spice Islanders, imetupa simanzi na majonzi, kama mnavyokumbuka leo ndiyo tunahitimisha siku ya tatu ya kufanya maombolezo ya kitaifa.
“Nawapongeza viongozi wetu kwa kuonesha ushirikiano wa hali ya juu ambao unathibitisha muungano wetu ni mfano wa kuigwa na Watanzania wote tulikuwa kitu kimoja katika msiba huu, Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi,” alisema
No comments:
Post a Comment