21 September 2011

Sumaye: Serikali ibadili mawazo kukabili tatizo la umeme nchini

Na Agnes Mwaijega

WAZIRI Mkuu mstaafu Bw. Frederick Sumaye, amesema kutokana na tatizo la umeme linaloikabili nchi kwa sasa, Serikali inapaswa kubadili mawazo ya kutegemea vyanzo
vya umeme vilivyozoeleka  badala yake itumie vyanzo vingine ili kumaliza tatizo hilo.

Bw. Sumaye aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika mdaharo uliokutanisha wadau mbalimbali wa nishati, madini na Miundombinu ambao uliandaliwa na sekta binafsi.

Alisema gharama za umeme wanazolipa wananchi kwa sasa ni kubwa hivyo Serikali ione umuhimu wa kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha tatizo lililopo linapatiwa ufumbuzi wa haraka.

Aliongeza kuwa, tatizo la umeme nchini limeathiri shughuli nyingi za maendeleo zinazotegemea nishati hiyo na kusababisha kushuka kwa uchumi wa nchi.

“Tatizo hili lisipopatiwa ufumbuzi, upo uwezekano mkubwa wa wawekezaji kuondoka, wananchi wanapaswa kuelimishwa juu ya tatizo lililopo ili watoe maoni yao,” alisema.

Akizungumzia miundombinu Bw. Sumaye alisema Serikali inatakiwa kubadili mfumo wa usafiri wa reli kama kweli inataka kukuza uchumi.

Alisema kama usafiri wa reli hautabadilika, nchi itakosa maendeleo kama inavyotegemewa hivyo lazima jitihada za makusudi zifanyike,” alisema.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini Bw. William Ngeleja, alisema Serikali pekee haiwezi kukabiliana na tatizo la umeme lililopo nchini hivyo ushiriki wa sekta binafsi unahitajika kumaliza tatizo lililopo.

1 comment:

  1. POROJO ZA NGELEJA ZA KULETA UMEME UTAIPONZA NCHI HII KWENDA KUZIMU. HAKUNA MIPANGO INAYOTEKELEZEKA. SHAME!!!!!!!!!

    ReplyDelete