*Pinda aionya TRA kuhusu rushwa
Na Grace Michael, Mara
SIKU nne baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuliagiza Jeshi la Polisi kuachana na vitendo vya kushiriki magendo ya sukari jeshi hilo
limekamata malori matatu yakiwa na mifuko 665 ya bidhaa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi jioni mkoani hapa na Kamanda wa Mkoa huo, Bw. Robert Boaz, wamiliki wa shehena hiyo wanahojiwa na hatua hiyo itakapokamilika hatua stahili zitachukuliwa.
“Operesheni hii imeanza leo (juzi) ambapo wafanyabiashara wanne tumewakamata wakisafirisha sukari hiyo kwenda nchi jirani na kama mkoa tumeamua kufanya operesheni maalumu ili kukabili tatizo hilo,” alisema ACP Boaz.
Aliwataja wafanyabiashara waliokamatwa kuwa ni pamoja na Mwere Nganshi, Peres Samwel, Boniface Francis na Andrew Nyambari ambao wako katika mahojiano na jeshi hilo.
“Hii mifuko ya sukari ilikuwa katika malori matatu yenye namba T.499 AET iliyokuwa na mifuko 235, T.972 EDL ikiwa na mifuko 210 na T.979 DCN ikiwa na mifuko 220...natoa onyo kwa wafanyabiashara wa sukari ambao watajihusisha katika vitendo vya kuvusha sukari nje ya nchi,” alisema Kamanda Boaz.
Alitumia mwito huo kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa kwa viongozi wa Serikali za Mitaa, wakuu wa wilaya, wakuu wa polisi wa wilaya na makamanda wa mikoa ya Mara na Tarime/ Rorya.
Hata hivyo, hatua hii ya kukamata shehena hiyo inazua maswali mengi kwa jamii kwa kuwa imefanyika baada ya kauli ya Waziri Mkuu ambaye aliweka wazi msimamo wake kuwa kama jeshi hilo limeshindwa kazi, serikali itatumia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ili kukabiliana na hali hiyo.
Kupanda kwa bei ya sukari imekuwa ni kero kwa Watanzania, hatua inayowafanya kutoa malalamiko kwa serikali kila kukicha.
Pinda aionya TRA
Waziri Mkuu Mizengo Pinda amewawataka watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutotumia vibaya mamlaka waliyopewa kukadiria kodi badala yake wautumie kwa maslahi ya taifa na si matumbo yao au kuwakwamua wafanyabiashara.
Amesema ili wananchi wapende wenyewe kulipa kodi kuna umuhimu wa watendaji hao kuongeza uaminifu na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Bw.Pinda alisema hayo jana mjini Tarime wakati akizindua Ofisi ya Mamlaka hayo wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Mara.
“Pamoja na mazuri mnayoyafanya kama TRA bado mnatakiwa mjimulike zaidi kwa kuwa naamini wapo watumishi ambao si waaminifu hata kidogo, kazeni macho, mwanya wa kukadiria mlionao msiutumie kwa kuwaumiza wananchi au kuwajengea mazingira ya rushwa,” alionya Bw. Pinda.
No comments:
Post a Comment