20 September 2011

Stars kuingia kambini Sept. 30

Kuivutia kasi Morocco

Na Zahoro Mlanzi

TIMU ya taifa 'Taifa Stars', inatarajia kuingia kambini Septemba 30, mwaka huu kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa mwisho wa Kundi D wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, mwakani (CAN 2012).


Taifa Stars katika kundi hilo, ipo nafasi ya tatu kwa pointi tano nyuma ya timu za Morocco na Jamhuri ya Afrika ya Kati ambazo zinazoongoza kwa pointi nane kila moja.

Timu hizo zinaongoza isipokuwa zinatofautiana mabao kufunga, huku Algeria ikiburuza mkia nayo ikiwa sawa na Stars isipokuwa imezidiwa kwa mabao.

Stars katika mechi hiyo inatakiwa kupigana kiume na kushinda mechi hiyo ili iweze kujiweka katika nafasi ya kushiriki michuano hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema timu hiyo itaingia kambini baada ya Kocha Mkuu, Jan Poulsen kuwasilisha programu yake na kupendekeza siku ya kuanza kambi.

"Maandalizi yanaendelea vizuri kuelekea mchezo wetu dhidi ya Morocco na tayari, Poulsen amewasilisha programu yake ambayo mbali na kupendekeza siku ya kuingia kambini, lakini pia inaonesha hakutakuwa na mchezo wa kirafiki na hii inatokana kuonekana kuwa na ugumu, kwani itakuwa si siku ya kalenda ya FIFA," alisema Wambura.

Alisema nchi nyingi zinajiandaa na mechi za mwisho za fainali hizo, hivyo hadhani kama zitapatikana kiurahisi, lakini watajipanga kuhakikisha timu inaandaliwa vizuri kwenda kuumana na Morocco. 

Mechi za kundi hilo zitachezwa saa 1.30 jioni siku moja ambayo ni Oktoba 9, mwaka huu ili kuepusha kupanga matokeo ambapo Taifa Stars, itakuwa jijini Rabat na Algeria itaumana na Jamhuri ya Afrika ya Kati Jijini Algiers.

Waamuzi wa mechi hiyo kati ya Stars na Morocco watakuwa ni Gassama Bakary, Jawo Dickory, Touray Sulayman na Camara Bakary, wote kutoka Gambia. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Zoumaro Gnofame kutoka Togo.

No comments:

Post a Comment