Na Addolph Bruno
KLABU ya Simba imeliomba Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kuruhusu mechi zao za Ligi dhidi ya Azam FC zichezwe katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
badala ya CCM Kirumba, Mwanza ambao Azam imependekeza kuutumia katika mechi zake za Simba na Yanga.
Hivi karibuni Azam FC inayomiliki Uwanja wa Chamanzi, Dar es Salaam ilipendekeza mechi zake kubwa hasa zinazohusisha vigogo hivyo kuchezwa Uwanja wa CCM kirumba.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Ofisa Habari wa Simba Ezekiel Kamwaga, alisema klabu hiyo ingependa kuona mechi hiyo inachezwa Dar es Salaam kama ilivyoelekezwa katika sheria ya TFF, kuwa klabu hairuhusiwi kuwa na viwanja viwili vya nyumbani.
"Simba tunaomba TFF, kama imepata barua kutoka Azam FC iliangalie vizuri suala hilo kwa mujibu wa sheria klabu hairuhusiwi kuwa na viwanja viwili vya nyumbani," alisema Kamwaga.
Kamwaga alisema wanafahamu kuwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam umefungwa kupisha matengenezo lakini alisisitiza kuwa TFF inaweza kuishawishi serikali kuruhusu na kuishauri kukubaliana na wazo hilo.
"Tunaomba serikali nayo ioneshe ushirikiano kwa maendeleo ya soka yetu, wakati mipango mingine inafanyika,"
Awali Klabu za Azam FC, Simba pamoja na Yanga zilichagua kuutumia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa ajili ya mechi zake za Ligi Kuu Bara, uwanja ambao serikali imeufunga kupisha matengenezo.
Kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo Simba itakipiga na Azam FC, Septemba 10 mwaka huu ambapo mchezo wa Azam dhidi ya Yanga utapigwa Septemba 18.
No comments:
Post a Comment