13 September 2011

Simba, Azam FC zaingiza mil. 72/-

Na Frank Balile

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), jana lilikusanya sh. milioni 72, 167,000, katika mechi kati ya Simba na Azam FC, iliyopigwa Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam, jana.

Katika mechi hiyo, timu hizo zilitoka suluhu, na kuiwezesha Simba kupanda kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa kujikusanyia pointi 10, huku ikiiacha JKT Ruvu kwa pointi moja nyuma.

Akizungumza mjini Dar es Salaam jana, Msemaji wa TFF, Boniface Wambura, alisema kuwa, fedha hizo zimepatikana kwa viingilio vya mashabiki waliokwenda kushuhudia mechi hiyo.

Wambura alisema watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo walikuwa 21,129, ambapo viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 15,000, sh. 7,000, sh. 5,000 na sh. 3,000.

Alisema kuwa, viti vya bluu na kijani ambavyo kiingilio chake kilikuwa  sh. 3,000, viliingiza watazamaji 18,586, na kuingiza sh. 55,758,000.

Wakatu huo huo, Wambura alisema kuwa, timu za Simba na Yanga zitaanza kuutumia Uwanja wa Azam Chamazi ulioko Mbande jijini Dar es Salaam wiki hii.

Simba watakuwa wa kwanza kushuka uwanjani hapo kuumana na Polisi Dodoma Septemba 14, mwaka huu, na Septemba 15, Yanga itakuwa mgeni wa African Lyon.

Alitaja viingilio kwa mechi zitazohusisha timu za Yanga na Simba kwenye uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 7,000, ni sh.15,000 kwa jukwaa kuu na sh. 5,000 mzunguko.

Kwa timu nyingine za Dar es Salaam zinazotumia uwanja huo, kiingilio kitaendelea kuwa kile kile cha sh. 10,000 jukwaa kuu na sh. 3,000 mzunguko.

No comments:

Post a Comment