Na Zahoro Mlanzi
KLABU ya Simba inatarajia kuvuna mamilioni mengine kutoka kwa beki wake ambaye pia huchezea 'Taifa Stars', Juma Nyosso baada ya kufikia muafaka na Klabu ya
Platnum Stars inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini, ambayo imeonesha nia ya kumsajili.
Timu hiyo ilituma ujumbe wake nchini kumalizana na Simba na kupata bahati ya kumshuhudia kwa mara nyingine beki huyo katika mchezo dhidi ya Stars na Algeria na baada ya kumalizika mchezo huo walitarajia kumalizia mazungumzo yao.
Mbali na hilo, klabu hiyo imejiwekea utaratibu kwamba wachezaji wake watauzwa kwenda timu nyingine kwa zaidi ya sh. milioni 100 kwani wana imani wanauzika.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam juzi usiku, mara baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya Stars na Algeria, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga alisema ni kweli wawakilishi wa timu hiyo ya Afrika Kusini wapo nchini wakiendelea na mazungumzo na timu yake kuhusu beki huyo.
"Tunashukuru Nyosso katika mchezo huu amejitahidi kucheza vizuri na tuna imani mambo yatakwenda vyema kama yalivyopangwa na yakiwa tayari hakuna shaka tutayaweka wazi kama tulivyofanya kwa wachezaji wengine," alisema Kamwaga.
Alisema kutokana na viwango vya wachezaji wao kuwa juu, watakubali kuruhusu mchezaji kuondoka hapo kwa gharama ya zaidi ya sh. milioni 100 na si vinginevyo.
Ofisa huyo alisema kutokana na uwezo wa Nyosso, ana imani klabu hiyo ya Afrika Kusini italiangalia kwa upana wake na kufikia muafaka ambapo kwa kufanya hivyo timu itazidi kujitengenezea sifa kwa kutoa wachezaji wengi nje ya nchini.
Mbali na hilo Simba ilimmwagia sifa aliyekuwa mshambuliaji wake ambye hivi sasa anakipiga Klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kideokrasi ya Congo (DRC), Mbwana Samatta kutokana na kiwango alichokionesha katika mchezo wa Stars na Algeria.
"Kama Simba tunampongeza Samatta kwa kudhihirisha ana kipaji cha hali ya juu kwa kufunga bao pekee, imetupa faraja kuona mchezaji wetu akifanya mambo makubwa kama yale," alisema Kamwaga.
Nyosso akifanikiwa kujiunga na timu hiyo, atakuwa amefuata nyayo za wachezaji wenzake Samatta, Patrick Ochan (wote wapo TP Mazembe) na Danny Mrwanda anayekipiga DT Long ya Vietnam.
Wengine ni Athuman Machupa anayecheza Sweden kwenye Klabu ya Vasuland IF na Mussa Hassan 'Mgosi' (DC Motema Pembe) ambapo klabu hiyo ilivuna mamilioni ya fedha kutokana kuwauza wachezaji.
No comments:
Post a Comment