05 September 2011

Sierra Leone yaivua ubingwa Misri

CANFREETOWN, Sierra Leone

MABINGWA watetezi ambao pia ni mabingwa mara saba, Misri wameshindwa kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (CAN 2012), ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha
miaka 30 iliyopita, baada ya kuambulia kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Sierra Leone.

Katika mchezo huo, uliofanyika juzi mjini Freetown,bao lililowekwa kimiani na mchezaji  Sheriff Suma dakika ya 14 na bao lililowekwa kimiani dakika ya 89 kwa mkwaju wa penalti na Mohamed Bangura,ndiyo yalihitimisha safari ya Mapharaoh hao kwenye michuano hiyo.

Kabla ya kuambulia kipigo hicho,Misri ilihitaji kushinda, ili iweze kupata nafasi ya kucheza fainali hizo za mwakani zitakazofanyika nchini Gabon na Guinea ya Ikweta.

Kipigo hicho kimekuwa ni cha tatu kwa Misri katika mechi tano na kimeifanya timu hiyo kushika nafasi ya mwisho kwenye kundi lake.

Hata hivyo kwa mujibu wa Shirika la Habari la Marekani (AP) hata kama Misri ingeshinda mechi hiyo ilikuwa bado ikihitaji ushindi mwingine ili iweze kuweka hai matumaini ya kutetea ubingwa wake katika fainali hizo.

Mchezaji Mohsen Maruwan ndiye aliyeisawazishia bao Misri dakika ya 45,lakini mkwaju wa penalti dakika za mwisho wa Bangura ndiyo ukazima ndoto za Mapharaoh hao ambao wanakabiliwa na mgogoro wa kisiasa nchini mwao.

Kwa ushindi huo wa pili mfululizo, Sierra Leone imekuwa na pointi sawa na viongozi wa kundi hilo Afrika Kusini na imejipa matumaini ya kufuzu fainali hizo.

Jana Afrika Kusini ilikuwa ikiumana na Niger katika mechi nyingine ya kundi G.

No comments:

Post a Comment