02 September 2011

Hotuba ya Kikwete yaibua angalizo

*Wataka vitendo zaidi vitumike kuliko maneno
*Askofu:Wauza dawa za kulevya washughulikiwe
*Mwingine aelezea suala la Mahakama ya Kadhi


Na Mwandishi Wetu

SIKU moja baada ya Rais Jakaya Kikwete kutumia Baraza la Idd El-Fitr, kuzungumza masuala mbalimbali yanayohusu mstakabali wa taifa, ambayo
baadhi yake yamekuwa yakiibua mijadala mikali nchini, baadhi ya viongozi wa dini wametoa maoni yao, wakiipongeza, lakini wakitoa angalizo kuwa iendane na vitendo.

Katika hotuba yake hiyo ya takribani dakika 65, juzi mjini Dodoma, Rais Kikwete alitumia muda huo kuzungumzia masuala mbalimbali kama vile uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, dalili za kuwepo kwa dhana ya udini nchini, hatima ya mali zilizokuwa zikimilikiwa na madhehebu ya dini kabla hazijataifishwa na serikali, ushiriki wa baadhi ya viongozi wa dini katika biashara haramu ya dawa za kulevya na mijadala ya katiba mpya.

Akizungumzia hotuba hiyo, Askofu wa Kanisa la African Inland Church (AICT), Dayosisi ya Pwani, Charles Salala, alisema kuwa hotuba ya Rais Kikwete katika Baraza la Idd, ilijikita katika masuala ya msingi, lakini katika baadhi ya hoja akatoa angalizo kuwa ni vyema serikali ikadhihirisha dhamira yake kwa vitendo badala ya kuishia katika maneno.

"Ni vizuri hili la serikali kutokuwa na dini liendelee kusimama katika uhalisia wake, serikali ilisimamie kwa uhalisia wake...katika suala la mahakama ya kadhi, moja ya vitu vilivyokuwa vikizungumzwa na wenzetu wa upande wa pili ni juu ya serikali kuhusika katika uendeshaji wa mahakama hiyo, kwa maana ya serikali kutumia fedha za walipa kodi ambao wengine wana dini wengine hawana dini, kuendesha chombo cha dini nyingine.

"Hilo likiwekwa vizuri kwa nini gharama hizo za kuendesha chombo zibebwe na serikali, maana karibu kila dini inazo gharama zake katika kuendesha masuala ya ibada, sasa isingekuwa sahihi serikali kugharamia ibada ya dini, ni vyema hilo likaendeshwa na wao wenyewe, serikali haina dini na ni vyema isimamie hilo kwa uhalisia wake.

"Juu ya suala la madawa ya kulevya kwa kweli hakuna mtu anaweza kutoka leo akasema kuwa halipo, categorically sidhani mtu anaweza kujitokeza na kuchukua position ya namna hiyo, maana huwezi kuwajua viongozi wote wa dini zote na malengo yao, lakini suaa la msingi ni kuwa hao wachache wanaojulikana serikali iwachukulie hatua, maana hakuna aliye juu ya sheria," alisema Askofu Salala na kuongeza;

"Serikali iwabainishe kwa kuwaweka wazi, iwachukulie hatua ili liwe funzo kwa watu wengine pia. Katika suala la katiba, ni kweli kabisa, katiba mpya inapaswa kutuuunganisha na kuwabeba Watanzania wote. Si mahali pa kila mtu kuweka maslahi yake mbele, yawe ya kidini au mengine yoyote yale, sisi tunaweza kuwa na tofauti zetu lakini katiba yetu ni moja tu, hiyo ibebe maslahi ya Watanzania wote, hivyo ni kweli tuwe makini."

Akizungumzia suala la dhana ya udini, Askofu Salala alisema kuwa ni vyema serikali nayo ikawa thabiti katika kuhakikisha kuwa hakuna viongozi wa dini wanaoendekeza udini, hasa katika mahubiri ambapo wamekuwa wakitumia muda mwingi kukashfu na kubeza dini za watu wengine, akisema viongozi wa dini wana mchango wao katika kumaliza tatizo la udini, lakini serikali isisite kuingilia kati na kuchukua hatua kukomesha vitendo vya namna hiyo.

Kwa upande wake, Padri Baptiste Mapunda alihoji kwa nini Rais Kikwete amechelewa namna hiyo kuzungumzia masuala muhimu kama hayo aliyoyasema jana. Lakini pia akahoji eneo ambalo rais aliamua kutolea ujumbe huo.

"Ataweza vipi kuthibitisha kuwa hayo aliyoyasema ndiyo yatafanyiwa kazi, maana suala lenyewe (la mahakama ya kadhi) haliendi kwa uwazi. Lakini kwa nini serikali ishiriki katika mchakato huo, kwa nini wasiachiwe waislam wenyewe, ina maana hawaamini waislam kama wanaweza kuanzisha mambo yao wao wenyewe, kwani hawawezi kujisimamia mpaka serikali iwasimamie," alihoji Padri Mapunda. 

8 comments:

  1. Jumuia ya Kiislamu ilikuwa itambue hili tangu asubuhi!!, si kulia kulia na kulalamika tu kama watoto wadogo hadi waelezwe kinaga ubaga kama hivyo walivyoumbuliwa! Zogo, kelele, wengine walikuwa tayari kuandamana maana ndio fashion! sasa hakuna pa kuweka uso!

    ReplyDelete
  2. Mim napata mashaka sana na baadhi ya binadamu wa tanzania,suala la mahakama ya kadhi linazungumziwa na maaskofu,how,mbona masuala ya jumuia ya dini ya kikristo huwezi kuona shehe akisimama na kulizungumzia?na kwa taarifa yako ww msemaji uliopita waislamu hawajaumbuliwa hizo ni siasa za jukwaan,kwan CCM waliposimama 2005 na kuahid kwamba watawasishia mahakama ya kadhi walikuwa ni watoto wadogo,we bwege kweli....hiyo ni ahadi ambayo Rais aliahidi.lazima watu waihoji.kama inakuuma kuwepo kwa mahakama ya kadhi,waweza pia azisha ya kwako pia.

    ReplyDelete
  3. na wewe hapo juu ninashangaa unapolalamika JK alishasema siku za nyuma kuwa kipengele cha kadhi kwenye ilani ya ccm kilichomekwa na mtu na yeye akuaidi jambo hilo. bahati mbaya wakati wa uchaguzi ndiyo lilikuwa eneo zuri la kumbana na msimamo wa swala hili kwani limekuwa likiendelea kwa miaka mingi lakini walikaa kimya wakimwani JK may be kwa uungwana wao au kwa sababu zao binafsi ingawa watu wengi walishasema JK haaminiki lakini hawakusikia.

    ReplyDelete
  4. Most of you Church goiners are either hamjui,jeuri au uchoyo wenu tu!!!
    Hivi mnajua mahospitali na mashule ya makanisa yanagharamiwa na serikali pia??!!!fedha ambazo ni za walipa kodi ambao waislam wakiwemo na matunda hayo ni ni ninyi ndio mnaofaidika!!Hakuna siku Serikali au kanisa wamekanusha hili!!!
    Hivyo madai ya waislam yana msingi.Waache wapewe hiyo ni haki yao.
    Kama mko serious enough ilazimisheni serikali iondoe ruzuku zote inazozigawia makanisa muone uhalisi wa mambo utakavyokuwa.

    ReplyDelete
  5. Ndugu zangu tunakokwenda siko, taifa hili tumekuwa wamoja kwa miongo mingi sasa inakuwaje tunashindwa kulinda amani na utulivu tulio nao.Mema mengi yamefanyika katika nchi hii kupitia madhehebu mbalimbali ya dini tuliyonayo,nakama tunataka kuwa wakweli iwapo tutaingiza tofauti za kidini ni wazi tunakoelekea nikatka kujichimbia shimo sisi wenyewe. BABA MUNGU NYOSHA MKONO WAKO TAIFA LINAKWENDA KUANGAMIA KWA UPUUZI WA WACHACHE WASIOKUBALI UKWELI

    ReplyDelete
  6. Mahosipitali ya kanisa yanasaidiwa na serikali kwa sababu sehemu kubwa ya bajeti ya Tanzania inaghalamiwa na nchi za ulaya ambazo ni za kikristo

    ReplyDelete
  7. ukataye mkubari. but ukweri anao JK mwenyewe kwamba YESU NI MUNGU.

    ReplyDelete
  8. anon wa sep 2 7.59 am, naomba utambue kuwa ukienda kwenye hospitali teule zamani za kanisa kutibiwa huulizwi dini yako.... hela zinazopelekwa huko ni kwa ajili ya dawa na mishahara wa watumishi ambao hawaajiriwi kwa kigezo cha dini...... wenzetu mnepunguza kasi ya kujenga misikiti na vituo vya petroli mngetufanyia la maana watanzania wenzenu ambaio tunashitaji huduma za msingi kama vile afya na elimu...mkifika hapo, na mkitoa huduma zenu bila ubaguzi mtakuwa mnastahili sapoti ya PUBLIC FUNDS!

    ReplyDelete