05 September 2011

Luhanjo kufungua tamasha la michezo Jumamosi

Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo, anatarajiwa kufungua tamasha la michezo litakalofanyika katika viwanja vya Sigara, Chang’ombe, Dar e Salaam Oktoba 10, mwaka
huu.

Tamasha hilo limeandaliwa na Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI), kwa lengo la utekelezaji wa agizo la Mkuu wa Utumishi wa Umma kuwahimiza watumishi kushiriki katika michezo ili kujenga afya zao.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa SHIMIWI, Ramadhan Sululu alisema tamasha hilo ni sehemu ya uzinduzi wa mashindano ya SHIMIWI mwaka huu yatakayofanyika jijini Tanga.

Alisema mashindano ya Taifa ya SHIMIWI yamepangwa kufanyika Oktoba 20 hadi Novemba 5 mwaka huu, mkoani humo.

“Ni matumaini yangu kwamba klabu zote vzitahudhuria na kufanikisha lengo la tamasha hili, karibuni tucheze pamoja kwa ajili ya afya zetu,” alisema Sululu.

Sululu alisema tamasha hilo pia litahudhuliwa na Makatibu wakuu na Manaibu wote kutoka Dar es Salaam na Dodoma, Makatibu Tawala wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, Wakuu wa Idara zote zinazojitegemea Mkoa wa Dar es Salaam, Watendaji wakuu wa Wakala wa Serikali na Wakurugezi wa Utumishi wa Utawala, Wizara na Idara zinazojitegemea Mkoa wa Dar es Salaam.

Wengine ni  watumishi wote kutoka katika Wizara, Idara zinazojitegemea,Wakala  wa Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Aliitaja michezo inayotarajiwa kuchezwa siku hiyo ni mpira wa miguu,netiboli na kuvuta kamba na Bendi ya Msondo Ngoma ‘Baba wa Muziki’, inatarajia kutoa burudani kwa washiriki wa tamasha hilo.

Aliongeza kwamba anatoa mwito kwa watumishi wote bila kujali jinsia zao kujitokeza kwa
wingi ili kuweza kufanikisha tamasha hilo.

No comments:

Post a Comment