27 September 2011

LALA SALAMA IGUNGA

Magufuli atinga kumnadi Kafumu

*Aelezwa ndiye bingwa kuzungumza Kisukuma
*CCM kutumia helkopta 2, mikutano 20 kwa siku


Na Benjamin Masese, Igunga
 
MAKADA maarufu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamezidi kumiminika katika
Jimbo la Igunga kusaidia kampeni za chama hicho huku Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli akitarajia kuwasili leo.

Waziri Magufuli anatarajiwa kuanza ngwe ya mwisho ya kumnadi mgombea wa CCM, Dkt. Dalaly Kafumu katika wiki ya lala salama kutokana na kujua lugha ya Kisukuma na kukubalika kwa wananchi wote nchini.
 
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana kutangaza hatua za CCM kumalizia kampeni zake, Mratibu wa Kampeni, Bw. Mwigulu Nchemba alisema lengo la kumuomba Dkt. Magufuli  ni kutokana na wananchi wengi wa jimbo hilo hasa maeneo ya vijijini kutofahamu Kiswahili vizuri na baadhi ya viongozi wanaojua Kisukuma wanapopanda majukwani kumnadi mgombea huonesha kueleweka zaidi.

Alisema CCM imekuwa ikipata shida ya kutoeleweka katika mikutano yake baada ya  wananchi kushindwa kuelewa Kiswahili.

Alisema wenzao wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamekuwa wakipata faida zaidi katika kampeni zake kwa kuwa Mbunge wa Maswa Mashariki, Bw. Sylvester Kasulumbayi amekuwa kivutio katika mikutano yake kwa kutumia Kisukuma.

Mbali na Waziri huyo, CCM kimewataja viongozi wengine watakaomnadi Dkt. Kafumu katika siku za mwisho kuwa ni pamoja na Mbunge wa Mtera, Bw. Livingstone Lusinde pamoja na Waziri wa Nchi, Mahusiano na Uratibu, Bw. Steven Wasira.
 
Bw. Nchemba alisema viongozi hao watawasili muda wowote kuanzia jana kuanza kampeni za wiki ya lala salama hadi Oktoba mosi mwaka huu.

Alisema kinachofikiriwa na CHADEMA kwa sasa, yaani matumizi ya helkopta, CCM ilikwishakifahamu na kukifanyia kazi wiki moja kabla.
 
Alisema wataalamu wa kufanya uchunguzi wa maeneo yanayofaa kutua helkopta wamesambaa jimbo zima kuweka alama na kazi hiyo ilitarajiwa kukamilika jana.

Bw. Nchemba alisema CCM inatajia kutumia helkopta mbili ambazo zimetolewa na wanachama wa chama hicho kwa lengo la kuhakikisha mgombea wao anaibuka na ushindi.
 
Kwa msaada wa helkopta hizo, alisema CCM itakuwa inafanya mikutano 20 kwa siku moja  hadi Oktoba Mosi zitakapoondoka kupisha wananchi kufanya maamuzi yao.

Wagombea watambiana

 
Wakati huo huo, wagombea wa CCM na CHADEMA wametambiana kwamba mmoja wapo akishindwa uchaguzi huo atapata kazi nyingine huku Dkt. Kafumu akisema anamhurumia Bw. Joseph Kashindye kwa kuwa 'ana elimu ndogo' isiyompatia kazi haraka.
 
Dkt. Kafumu alisema ikiwa atashindwa atarudi kufundisha vyuoni kwa kuwa ana elimu ya juu (Phd) ya masuala ya madini.

Pia alisema ataanzisha taasisi ya utafiti wa madini na kuajiri vijana na kuongeza kwamba amekuwa akitafutwa na wamiliki wa makampuni makubwa ya madini, hivyo uwezekano wa kuajiriwa siku moja baada ya uchaguzi upo.
 
Naye Bw. Kashindye alisema hatarajii kushindwa uchaguzi, ila ikitokea bahati mbaya anatarajia kwenda kufundisha shule za binafsi kwa kuwa wanamhitaji.
 
Alisema akiwa kama mtu mwenye taaluma ya ualimu hivi sasa ana mpango wa kuanzisha shule ili kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wa Igunga ili kuondokana na adui ujinga.
 
Wagombea hao walitambiana jana asubuhi kwa nyakati tofauti walipofutwa na mwandishi wa habari hizi kuelezea matarajio yao baada ya uchaguzi.

7 comments:

  1. WANAIGUNGA, WATANZANIA TUNAWASIHI MSITILIE MAANANI MATAKAYOELEZWA SAA HIZI ZA MWISHO NA VIGOGO WANAOMIMINIKA KUTOKA DAR ES SALAAM. WASIKILIZENI ZAIDI WALE VIONGOZI WENU WANAOISHI NA NYIE VIJIJINI. HAWA WANATAMBUA SHIDA, MANYANYASO, UFISADI, MATUMAINI YENU KIUCHUMI , KIAFYA KIELIMU N.K. HAWA WATAWAWEZESHA KUTOA UAMUZI WA NANI WA KUMPIGIA KURA. BENDI , MAHELIKOPTA, MAGARI YA KIFAHARI, VUVUZELA HAZITAWASAIDIA. vIGOGO HAWA HAWA NDIO WANAOOWASABABISHIA UMASKINI. HAWA NDIO WANAOSHIRIKI UMASIKINI. hATA KAMA WANAJUA KISUKUMA KULIKO NYIE ACHANANI NAO. WATAZUNGUMZA NANYI KWA DAKIKA CHACHE NA LABDA KAMWE HAMTAWASIKIA AU KUWAONA TENA LABDA KWENYE REDIO NA LUNUNGA. pIGENI KURA ZENU KWA AMANI NA MHAKIKISHE KURA ZENU HAZITACHAKACHULIWA!

    ReplyDelete
  2. TUOMBE MUNGU UCHAGUZI UISHE SALAAMA NA MAISHA YA WANANCHI YAENDELELEE KWA AMANI.KUNA JAMBO NAPENDA KUIULIZA SERKALI HIVI MBONA KESI YA EPA TUNAYO ISIKIA NI MOJA TUU YA KINA MARANDA ZINGINE ZIMEZIMWA?
    MBONA HAZISIKI TENA JEE KULIKONI

    ReplyDelete
  3. Tusikubaliane na siasa za ukabila kamwe. Tanzania ni moja hakuna kampeni za Kisukuma huku ni kujenga chuki kwani wana-Igunga wote si Wasukuma. Lugha ya taifa ni kiswahili. Tume iwe macho la hili vinginevyo........................!!!!!!!

    ReplyDelete
  4. Kama tujuavyo Leo hii tukipiga kura hapa igunga 1:CCM 2:CUF 3:CDM Tunashukuru kwamba Dr Kafumu kweli anastahili angalia alivyokuwa ametulia wakati wa Mdahalo hakuwa na wasiwasi yeye alicheza na kuongozwa na ilani ya CCM; wenzangu na mimi kama kawaida na Bendi yao maarufu ya Udaku na Mipasho iliendelea mpaka ukumbini hapo,Vijana tunarubuniwa tutawezeshwa kupata Ajira wakati tupo kama Mahona inakuwaje? Kafumu ndiye atakayewasaidia Vijana wa Igunga Kujiajiri wenyewe badala ya kupoteza muda kusubiri CDM eti wanazo ajira mbona hawazitoi? Mwenye macho haambiwi Tazama;

    ReplyDelete
  5. NCHI TAYARI ITAFIA MIKONONI MWA KIKWETE HUYU RAIS WA NAMNA GANI JAMANI! KAMPENI KWA KISUKUMA? HALAFU BILA AIBU WANASEMA WANAMLETA WAZIRI ANAYEJUA KISUKUMA! SIKUBALI HILI! NAPINGA

    ReplyDelete
  6. kukosa mwelekeo kwa taifa ndio huku? Sasa wanyemwezi, wahehe, wapare, wachaga, wamakonde, na makabila mengine yanaoishi Igunga nao wataletewa mawaziri wanaozungumza lugha zao? Raisi uko wapi hadi watu wanafanya kampeni za kikabila? CCM huku ndio kumuenzi Mwalimu? Ukabila? Kha! Kweli kuchagua Raisi tuache mizaha! Raisi anaweza kuokoa au kuangamiza Taifa! Tusifanye mzaha 2015

    ReplyDelete
  7. Hivi mbona Zanzibar kimya? kwani si tumefiliwa na Mwakilishi/Mbunge? mbona ZEC hawafanyi uchaguzi? tunalitaka timbwili la asha ngedere na sisi!!

    ReplyDelete