07 September 2011

'Rais sasa asiwe mwenyekiti CCM'

*Yaelezwa chama kimekosa uwezo kukosoa serikali
*Mawaziri, ma-RC, ma-DC nao waondolewe ujumbe NEC


Na Mwandishi Wetu

HALI ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) si shwari kutokana na misuguano ya makundi hali inayosukuma baadhi ya
makada wake wakongwe kupendekeza kutenganishwa kofia mbili urais na uenyekiti wa chama ili kutoa nafasi pana kwa chama kufuatilia na kukosoa kasoro za utendaji wa serikali.

Misuguano hiyo imetokea ikiwa imebaki takribani miezi mitatu kabla ya kuingia mwaka 2012 utakapofanyika uchaguzi mkuu wa chama hicho tawala.

Imeelezwa kwamba pamoja na baadhi ya viongozi ndani ya chama hicho kukanusha kuwepo makundi, hali hiyo sasa ni bayana sambamba na chama hicho kuzidi kushindwa kuikosoa serikali kutokana na viongozi wake kuvaa kofia mbili kwa wakati mmoja.

Sambamba na kutenganisha kofia ya urais na uenyekiti wa chama pia watendaji wengine wa serikali wakiwemo mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya wametakiwa kutokuwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) na 'kushika moja' ili kuimarisha chama hicho.

Kuzidi kuporomoka kwa uchumi wa nchi ni mambo yanayoelezwa kuchangiwa kwa njia moja ama nyingine na mtu mmoja kuwa na kofia mbili muhimu yaani urais na unyekiti wa chama hali inayosababisha chama kukosa macho ya kuona udhaifu wa serikali na kuurekebisha.

Akizungumza na gazeti kwa sharti la kutotaja jina lake kwa sasa, mmoja wa wanasiasa wanaoheshimika nchini na mwenye uzoefu mkubwa wa shughuli za chama ambaye pia aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, alisema kama CCM inataka kuendelea kushika hatamu suala la kutenganisha kofia mbili sasa haliepukiki.

Alisema hali si shwari ndani ya chama hicho na muda ukifika hakuna atakayeona woga wala haya kubainisha ukweli huo kwa kuwa ndio njia pekee kukinusuru chama hicho na serikali kutokana na mitikisiko inayoendelea.

Akaongeza kwamba hata hivyo, CCM imechelewa kuchukua hatua hiyo, na ili kujaribu
kujinusuru, jambo hilo lifanywe haraka kwenye mkutano mkuu wa chama hicho mwakani
kwa nia njema na hatua hiyo isichukuliwe kuwa ina lengo la kumkomoa au kumhujumu mtu
fulani.

"Inasikitisha sana kwamba ndani ya chama chetu watu hawataki kusikia kuwa kuna mgawanyiko mkubwa, tunamdanganya nani? Nani haoni kuwa chama chetu sasa kimeyumba kwa kiasi kikubwa na kimeshindwa kuisimamia serikali yetu katika utendaji wake na kuleta maisha bora. Kila kukicha watu wanalia maisha magumu, bei za bidhaa madukani hadi vyakula zinapanda, angalia sukari hakuna kinachoeleweka." alisema.

"Pale Dodoma White House kwenye ukumbi wetu tumebandika wosia wa Mwalimu (Baba wa Taifa Julius Nyerere) wakati anang'atuka, umewahi kuona? (alimuuliza mwandishi) Mwalimu alisema hivi; 'Mimi nang'atuka lakini nitaendelea kuamini kuwa bila CCM madhubuti nchi yetu itayumba," alimnukuu Mwalimu na kueleza kwa msisitizo "nenda kasome yapo pale ukutani.

Alikishambulia chama hicho kwa maelezo kwamba kimekosa mvuto jambo linalomfedhehesha hata yeye na kubainisha kuwa CCM sasa ni kambi ya malumbano na makundi ambapo viongozi wake wanaishi kwa kuvumiliana lakini si kwa imani ya chama na umahili wao katika kusimamia na  kutekeleza malengo ya chama hicho.

Alisisitiza pia kufanyika marekebisho ya kutenganisha kofia hizo kwa mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya kujivua wadhifa wa ujumbe wa NEC ili kukipa nafasi chama kusimamia utendaji wao.

"Leo unakuta waziri, mkuu wa mkoa au wilaya ni mjumbe wa NEC, nani atamnyooshea mkono akiharibu? Kwa mfano leo hii Maghembe (Prof. Jumanne) ni Waziri wa Kilimo na Mjumbe wa NEC Kilimanjaro, Mwandosya (Prof. Mark) ni Waziri wa Maji na m-NEC Mbeya, Membe (Benard ) ni Waziri wa Mambo ya Nje na m-NEC Lindi, Nagu (Dkt. Mary ) ni Waziri wa Uwezeshaji na m-NEC  Manyara,  Lukuvi( William) ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge)  m-NEC Iringa, sasa wakikosea chama kitawanyooshea kidole?"

"Naijua saana nchi hii na chama hiki(CCM). Angalia yanayoendelea, tumegeuka kundi la waimba taarabu, kinachofanyika ni malumbano hakuna kazi za chama, kila anayesimama ni kurusha vijembe, huyu akitoa kauli mwingine anampinga, yanazuka malumbano," alisema na kuongeza kuwa kujivua gamba ndani ya chama hicho kungekuwa na ufanisi zaidi kama ungesimamiwa na mwenyekiti ambaye si Rais wa nchi.

Naibu Katibu Mkuu wa CCCM Tanzanian Bara, Bw. John Chiligati na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa NEC, Bw. Nape Nnauye hawakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo. Simu ya Bw. Nape ilipopigwa jana ilipokelewa na mtu aliyesema sema kuwa kiongozi huyo wa CCM alikuwa kwenye mkutano kwa mrefu.

2 comments:

  1. Mheshimiwa huyu lazima atambue kuwa CCM aliyosema Nyerere kuwa bila hiyo nchi itayumba siyo CCM hii ya leo hii. CCM ya leo haijali watu kazi yao kubwa ni kuwalinda wezi na wabadhirifu wakubwa kama akina CHENGE, ROSTAM, LOWASSA NA WENGINEO WENGI. NI AIBU SANA NA NI KUMFEDEHESHA NYERERE KUMUHUSISHA YEYE NA CCM HII YA SASA KWA MAANA NYERERE ALIKUWA HANA URAFIKI NA WEZI NA WABADHIRIFU WA UCHUMI.

    ReplyDelete
  2. Ndiyo kabisa bwn hamis,Lakini jamaa wa hapo juu amesema,NYERERE ALISEMA BILA CCM MADHUBUTI NCHI HII ITAYUMBA!!Na kweli nchi hii inayumba kwani CCM ya sasa si madhubuti,mchonga alikuwa anaona mbali

    ReplyDelete