30 September 2011

Papa Benedict 16 afurahishwa na amani ya kidini Tanzania

Na Mwandishi Wetu

KIONGOZI wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Papa Benedict wa 16, ameeleza kufurahishwa na kuridhishwa na amani, utulivu na uvumilivu wa kidini ulioko
nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,Ikulu jana, licha ya kuwepo kwa imani tofauti za kidini lakini watanzania wameonyesha upendo na maani na utulivu bila kubaguana jambo ambalo ni tunu.

Pamoja na kutaka kujua siri ya mafanikio ya utulivu na uvumilivu huo wa kidini Tanzania, Baba Mtakatifu pia amewapongeza viongozi wa nyanja na sekta mbalimbali kudumisha hali hiyo na kuwataka kuendeleza kushikilia siri ambayo imedumisha utulivu huo kwa miaka 50 tokea uhuru.

Msimamo huo wa Papa Benedict wa 16 ulitolewa jana na Balozi wa Makao Makuu ya Baba Mtakatifu ya Vatican nchini Mhashamu Askofu Mkuu Joseph Chennoth, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete Ikulu, Dar es Salaam.

Mhashamu Askofu Mkuu Chennoth alikuwa anamuaga Rais Kikwete baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi wa Vatican nchini.

Askofu huyo amekaa nchini miaka sita ikiwa ni sehemu ya miaka 15 ambako ameiwakilisha Vatican katika nchi mbalimbali za kiafrika.

Balozi Chennoth ambaye aliwasili nchini Agosti 22, mwaka 2005 anahamishiwa nchini Japan.

“Siku zote Baba Mtakatifu amekuwa anaulizia juu ya siri ya mafanikio ya uvumilivu wa kidini katika Tanzania.

Kwa hakika, Baba Mtakatifu anatambua hali hii, anawapongeza viongozi wa Tanzania kwa kulisimamia na pia anaombea hali hii iendelee kuwepo katika Tanzania,” alisema Balozi Chennoth katika mazungumzo yake na Rais Kikwete.

Balozi pia amesifia ushirikiano uliopo kati ya viongozi wa dini na wa siasa na kutaka hali hiyo idumishwe kwa maslahi ya taifa.

“Sisi siyo washindani, siyo wapinzani. Sisi ni wabia na washiriki katika shughuli za kuwahudumia wananchi na kuwafikishia huduma za kijamii.

Tunashirikiana katika utoaji elimu, katika utoaji huduma za afya na huduma nyingine za kiroho na kimwili. Kwa kweli imekuwa ni faraja yangu kubwa kutumikia katika nchi hii yenye historia ya kutukuka duniani, nchi ya Mwalimu Kambarage Nyerere,”alisema Askofu huyo.

Kwa upande wake Rais Kikwete alimpongeza Askofu huyo kwa kukuza uhusiano kati ya Tanzania na Vatican katika kipindi chake cha uwakilishi nchini.

“Umesaidia sana kuimarisha uhusiano kati ya Vatican na nchi yetu, kati ya umoja wa Kikatoliki duniani na wananchi wetu, Tunakushukuru sana,”alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete pia amesifia uhusiano uliopo kati ya Serikali ya Kanisa Katoliki na kuwataka viongozi wa kisiasa na kidini kukumbuka kuwa wao wanayo dhamana kubwa ya kuendeleza uhusiano huo na kudumisha uvumilivu wa kidini nchini.

“Ni wajibu wetu viongozi wa kisiasa na wa kidini kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa ya amani na tunaendelea kuishi kwa namna hii ya kuvumiliana.

Jukumu hili liko mikononi mwetu, Tukivuruga utulivu huo tutakuwa tumeivuruga nchi yetu kwa namna ya kudumu hatutaupata tena utulivu huo kwa sababu ni vigumu sana kuutengeneza upya,”alionya Rais Kikwete.

Rais Kikwete pia ametumia nafasi hiyo kumkumbusha Balozi Chennoth kuhusu mwaliko wake ambao aliutoa kwa Baba Mtakatifu wakati alipotembelea Vatican mwaka 2008.

“Nilimpa mwaliko Baba Mtakatifu wakati tulipokutana Vatican wakati wa ziara yangu aliponialika nimtembelee na baada ya hapo tulipokutana mjini Napoli. Bado Wakatoliki wa Tanzania na Watanzania kwa jumla wanaendelea kumsubiri,”alisema.

No comments:

Post a Comment