14 September 2011

Ndege yaanguka Mbeya wanne wanusurika kifo

Ndege ndogo ya kukodi aina ya CESSINA 9J-BIO ikiwa imeanguka katika shamba la mahindi maeneo ya Uyole jijini Mbeya jana. Watu wanne waliokuwa wakisafiri na ndege hiyo wamenusurika katika ajali hiyo. Mmoja wa abiria hao ni Balozi mstaafu, Bw. Mohamed Ramia.
*Yumo Balozi Mohamed Ramia

Na Rashid Mkwinda, Mbeya

IKIWA ni siku ya tatu ya maombolezo ya watu zaidi ya 200 waliokufa baada ya kuzama kwa
meli ya MV Spice Islanders, Visiwani Zanzibar, watu wanne jana walinusurika kufa akiwemo Balozi mstaafu Bw. Mohamed Ramia.

Watu hao walinusurika baada ya ndege ndogo waliyokuwa wakisafiria kutoka  Mbeya kwenda jijini Dar es salaam kuanguka katika shamba la mahindi eneo la Uyole jijini hapa.

Taarifa za mwanzo za tukio hilo zilidai kuwa ndege hiyo ndogo yenye namba za usajili 9J-BIO CESSINA 206  ilikuwa na watu wanne,wakiwemo wawekezaji wa  kampuni ya Export Trading Company, ambayo inaendesha Shamba la Kapunga lililopo wilayani Mbarali mkoani humo.

Ajali hiyo ilitokea majira ya saa mbili asubuhi baada ya ndege hiyo kukosa mwelekeo uliosababishwa na hali ya hewa eneo kubwa la Jiji la Mbeya ambako kulikuwa na upepo mkubwa.

Akizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya Anacletus Malindisa alisema chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana

Lakini rubani wa ndege hiyo Bw.Jver Waak alisema chanzo cha ajali hiyo ni hitilafu iliyotokea katika injini  kisha kupoteza mwelekeo na kuanguka.

Aliwataja watu walionusurika katika ajali hiyo kuwa ni pamoja na rubani wa ndege hiyo, Bw. Waak (49)ambaye ni raia wa Afrika Kusini, Balozi Mohamed Ramia (64), Bw.Christian Mmasi (30) ambaye ni ofisa utawala wa shamba la Kapunga, pamoja na Bw.Sunil Tahil (50)Meneja wa mashamba hayo ya Kapunga.

Hata hivyo kamanda Malindisa alisema kuwa katika ajali hiyo, hakuna aliyepata majeraha yeyote au kupoteza maisha mbali ya baadhi yao kupata mshtuko.

Katika eneo hilo la tukio kumekuwa na mfululizo wa ajali za ndege ndogo ambapo miezi saba iliyopita ndege ndogo ilianguka na kusababisha kifo cha mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Swilla iliyopo Mbeya Vijijini mkoani hapa.

Ndege nyingine ndogo kama hiyo iliwahi kuanguka na kusababisha kifo cha mtu mmoja Godfrey Mpoli, aliyekufa papo hapo na wengine watatu kujeruhiwa vibaya.

No comments:

Post a Comment