Maiti 5 zaokotwa baharini Mombasa
*Bahari yachafuka, wazamiaji washindwa kuanza kazi
*Misaada yazidi kumiminika kwa waathirika wa ajali
Na Mwajuma Juma, Zanzibar
MIILI mitano ya watu watano waliokufa kwa ajali ya Meli Mv Spice Islanders iliyozama katika
Mkondo wa Nungwi wiki iliyopita imeokotwa katika maeneo ya Mombasa Kenya.
Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, alithibitisha habari hizo alipokuwa akipokea misaada kutoka kwa taasisi mbalimbali ofisini kwake Vuga mjini hapa.
Kuokotwa kwa miili hiyo kunaongeza idadi ya watu waliokufa na kufikia 245 hadi jana.
Balozi Seif alisema kuwa miili hiyo ilionekana juzi katika maeneo hayo ya
Kenya, na kuzikwa huko huko kutokana na kuharibika vibaya.
Hata hivyo Balozi Idd alisema taarifa ya kuokotwa kwa miili hiyo
zilithibitishwa na Balozi Mdogo wa Tanzania aliyeko Kenya Bw. Yahya Haji
Jecha na kusema kuwa Serikali inaendelea kuwasiliana na maeneo mbalimbali ili kuona kama kuna miili ya watu wengine iliyoonekana.
“Tupo pamoja na inshahallah tuwaombee marehemu hawa na pia tunatarajia kupata maiti nyingine zaidi, kwa hiyo bado shughuli za uokozi zinaendelea”, alisema.
Habari zilizopatikana jana zinaeleza kuwa kazi ya kutafuta miili zaidi kwenye meli iliyozama ilishindikana kuanza jana baada ya wazamiaji waliowasili kutoka Afrika Kusini kushindwa kuanza kazi hiyo kutokana na bahari kuchafuka.
Balozi Seif Idd alithibitisha habari za wazamiaji hao kushindwa kuanza kazi jana lakini hakueleza zaidi sababu za kufanya hivyo.
Katika tukio hilo Balozi Seif alipokea msaada wa shilingi milioni 30 kutoka kwa Jumuiya yak OJA Shiya kutoka Shirikisho la Afrika ambao walisema msiba huo ni wa wote na kuungana na Watanzania katika kipindi hiki cha msiba.
Rais wa Shirikisho hilo Alhaj Anuwar Dharamshi alisema msaada huo waliotoa ni kwa ajili ya kusaidia ndugu za waliopoteza maisha katika ajali hiyo ya meli.
Aidha wajumbe wa Baraza la wawakilishi nao walitoa rambirambi kwa Serikali na kukabidhi sh. milioni 15 kwa Makamu wa Pili wa Rais huyo, ikiwa ni mchango wao katika kusaidia shughuli mbalimbali za msiba huo wa taifa.
Aidha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa shilingi milioni 10, fedha ambazo zilikabidhiwa na Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bw. Wilson Mukama.
Wengine waliochangia maafa hayo ni wabunge wa Afrika Mashariki wa Tanzania ambao walitoa sh. 2,000,000 zilizokabidhiwa kwa niaba ya wabunge hao na Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi Bi. Mgeni Hassan Juma.
Katika hatua nyingine Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa itatoa tamko rasmi kuhusu uzushi wa kuwa imekaata misaada ya kampuni ya Vodacom.
Waziri wa Nchi Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais Bw. Mohammed Aboud alisema kuwa kwa sasa hawezi kuzungumza chochote kuhusu uvumi akiahidi kuwa angetoa tamko baadaye.
“Tamko rasmi litatolewa baadae kuhusu suala hili”, alisema Waziri Aboud.
Kumekuwepo na uvumi juu ya taarifa hiyo, ambapo inadaiwa kuwa Serikali imekataa msaada wa Kampuni ya Vodacom.
Uvumi huo umeenea katika maeneo yote ya Zanzibar ingawa hazijaelezwa ni
sababu gani zimeifanya uvumi huo wa kukataa msaada huo uenee.
Issue si zanzibar ni mtazamo wa kila mtanzania kwenye usafiri, kiti cha watu wanne pale arusha moshi wanakaa sita, ukisema ,jamani nabanwa unaambiwa nunua gari lako. Tunahitaji waziri mmoja kama michuki wa kenya na atakayethibiti traffic police. watz wengi bado hatufahamu haki zetu tuko kwenye uji..nga na ujima. Hata ninyi mnaolaum serikali jana mlipanda daladala zilizojaa. think about it!
ReplyDelete