29 September 2011

Mkuchika amweka kikaagoni DC Rombo

Na Martha Fataely, Rombo

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Bw. Geroge Mkuchika amekataa taarifa ya Mkuu wa Wilaya ya
Rombo, Bw. Peter Toima iliyokuwa ikieleza jinsi walivyofanikiwa kudhibiti chakula na sukari kusafirishwa nje ya nchi kwa njia ya magendo.

Bw. Mkuchika ambaye ameanza ziara ya siku mbili mkoani Kilimanjaro katika wilaya za Rombo na Mwanga, alikataa taarifa hiyo akidai ni uongo.

Katika taarifa yake kwa Bw. Mkuchika, Bw. Toima  alisema wilaya hiyo kupitia timu maalumu imefanikiwa kudhibiti mahindi na sukari kupelekwa kuuzwa nje ya nchi.

Alisema walifanikiwa kukamata mifuko 200 ya sukari yenye ujazo wa kilo 50 kwa kila mfuko.

Mkuu huyo wa wilaya alisema baadhi ya vyombo vya serikali ikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Polisi na wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakikiuka maagizo halali ya serikali na kusaidia usafirishaji kwa njia haramu chakula hicho.

“Kutokana na kubaini mapungufu hayo serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwamo kuwafukuza kazi watendaji hao....pia jeshi la polisi limefanya mabadiliko ya maofisa wake ambapo Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) na Mkuu wa Upelelezi OC-CID wamehamishwa,” alisema Bw. Toima.

Alisema baada ya kukamata sukari hiyo wilaya inafanya mipango kwa kuiuza kwa bei elekezi ya serikali isiyozidi sh. 1,800.

Alisema wilaya imeunda kikosi kazi maalumu wa ajili ya kufuatilia bei ya sukari katika maduka ya reja reja ingawa kwa sasa bidhaa hiyo huuzwa wastani wa sh. 2,000 hadi 2200 kwa kilo moja huku bei elekezi ikiwa Sh 1,700.

Katika majibu yake kwa mkuu wa wilaya, Bw. Mkuchika alisema kama wilaya hiyo ingefanikiwa kudhibiti usafirishwaji wa sukari isingeuzwa kwa bei ya sh.
2,000 hadi 2,500.

Aliutaka uongozi wa wilaya kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa, Bw. Leonidas Gama kuhakikisha hakuna chakula wala sukari inayosafirishwa kwenda nje ya nchi.

3 comments:

  1. mheshimiwa mkuchika angekuwa na taarifa tofauti na ya dc ingetuwezesha kujua sababu ya kukataa taarifa hiyo. vinginevyo hii ni dalili ya ubabe na kumdhalilisha dc kwa kusema taarifa yake ni ya uongo. bei ya madukani inategemea muuzaji. ni vyema viongozi wa serikali wakawa waangalifu na wanachokisema kwani wananchi nao wana akili ya kuchambua mambo na ndiyo wanaoumia na utendaji mbovu wa serikali.

    ReplyDelete
  2. mheshimiwa mkuchika angekuwa na taarifa tofauti na ya dc ingetuwezesha kujua sababu ya kukataa taarifa hiyo. vinginevyo hii ni dalili ya ubabe na kumdhalilisha dc kwa kusema taarifa yake ni ya uongo. bei ya madukani inategemea muuzaji. ni vyema viongozi wa serikali wakawa waangalifu na wanachokisema kwani wananchi nao wana akili ya kuchambua mambo na ndiyo wanaoumia na utendaji mbovu wa serikali.

    ReplyDelete
  3. sasa limegeuka mambo sukari kapewa deler mmoja tu ambaye ni mtoroshaji mubwa zaidi

    ReplyDelete