Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Habari Tanzania (MCT), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, leo wataadhimisha siku ya kimataifa ya 'Haki ya Kujua', ili jamii kubwa iweze kujua haki zao
za kupata habari kutoka serikalini na taasisi binafsi.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Katibu Mtendaji wa MCT, Bw. Kajubi Mukajanga, imesema siku hiyo huadhimishwa ifikapo Septemba 28 kila mwaka.
“Huu ni mwaka wa tisa tangu siku hii iliposainiwa na wanaharakati wa kutetea haki ya kupata habari katika mkutano wao uliofanyika nchini Bulgaria mwaka 2002 na kuadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2003,” alisema Bw. Mukajanga.
Alisema MCT itatumia siku hiyo kusisitiza misingi mikuu ya 'Haki ya Kujua', ambayo inasema, kupata habari ni haki ya kila mtu, uwazi utawale maisha, usiri ndio uwe kitu cha ajabu, haki ya kupata itekelezwe na taasisi zote za umma, maslahi ya taifa yawekwe mbele badala ya kutetea usiri.
Misingi mingine ni kila mtu ana haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi unaokwaza upatikanaji habari, watumishi wa serikali na taasisi za umma wana wajibu wa kuwasaidia wananchi wanaoomba taarifa, utaratibu wa wananchi wanaoomba taarifa unatakiwa kuwa mwepesi, wa haraka na bure na ombi la habari linapokataliwa ziwepo sababu za msingi za kufanya hivyo.
Nyingine ni taasisi za umma zitangulie kutangaza habari muhimu badala ya kusubili ziombwe na kuwepo taasisi huru ya kuhakikisha haki ya kupata habari inalindwa.
“Maadhimisho haya yatajumuisha mijadala katika vyombo vya habari yakiwemo magazeti, radio na televisheni, pia kutakuwa na kongamano ambalo litashirikisha wadau wa habari na Serikali, utaratibu wa mijadala katika vyombo vya habari unafanywa na MCT kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la HakiElimu,” alisema.
Bw. Mukajanga aliongeza kuwa, kimataifa maadhimisho hayo yana ujumbe unaosema “Upatikanaji wa habari kwa wananchi ndiyo njia yab kuelekea katika maendeleo: Una Haki ya Kujua”
Alisema katika kongamano hilo, mada kuu itakuwa “Umuhimu wa haki ya kupata habari katika kuimarisha demokrasia na utawala bora” ambapo siku hiyo, huadhimishwa duniani kote ili kuhamasisha wananchi kudai sheria ambazo zitahakikisha kunakuwepo uhuru na haki ya kupata habari.
Maadhimisho hayo pia hutumika kutoa taarifa kwa wananchi jinsi ya kutumia sheria za upatikanaji habari katika nchi zenye sheria hizo.
No comments:
Post a Comment