19 September 2011

Mbatia akingiwa kifua asing'olewe

Na Godfrey Ismaely

KATIBU Mkuu wa chama cha NCCR Mageuzi Bw.Samwel Ruhuza, amemkingia kifua  mwenyekiti wa taifa, Bw. James Mbatia, ambaye baadhi ya makada wa chama hicho
wanashinikiza ajiuzulu wadhifa huo.

Makada hao wanadai kiongozi huyo ni kibaraka wa CCM kutokana na kutoa matamko yanayokinzana na vyama vya upinzani.

Katibu huyo alienda mbali zaidi na kusema kuwa  katiba ya NCCR-Mageuzi haioneshi ukomo wa kiongozi aliyeko madarakani, ambaye amechaguliwa kwa ridhaa ya wanachama kujiuzulu.

Alisema katiba inasema mwanachama yeyote atakayekiuka kanuni za nidhamu ndani ya chama atachukuliwa hatua.

Bw. Ruhuza aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akihojiwa katika kipindi cha Mambo Leo kilichotangazwa na Redio Times Fm (100.5).

Alisema hawezi kulizungumzia suala la Kamishina wa chama hicho Mkoa wa Tanga, Bw. Mbwana Hassan, kwa  kumtuhumu Bw. Mbatia  na kumtaka kujiuzulu.

"Suala la kujiuzulu madaraka si kama wanavyofikiria pia kila mtu anayo haki ya kuwa na mawazo yake ,lakini yenye uhalisia wa ukweli ukiwamo ushahidi wa kutosha," alidai Bw. Ruhuza.

Akizungumza na Majira, Kamishina wa chama hicho Mkoa wa Tanga,Bw. Hassan, alisema Bw. Mbatia anachangia chama hicho kupoteze imani kwa wanachama wake.

“Mimi ni mmoja wa wazee waliokutana na Bw. Mbatia Julai 28, mwaka huu na kumshauri ajiuzulu nafasi aliyonayo,tulimweleza yale yanayosemwa na watu mikoani, maendeleo ya chama chetu na kauli anazotoa katika vyombo vya habari.

Naye Willbroad Mathias anaripoti kuwa Katibu  Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Bw.Kamalesh Sharma amemwalika Mbunge wa Jimbo la Ubungo,kwa tiketi ya CHADEMA, Bw.John Mnyika, kwenda nchini Zambia kwa ajili ya  kuangalia shughuli ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unatarajiwa kufanyika kesho nchini humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwenye vyombo vya habari kupitia mtandao wa sekretariati ya jumuiya  hiyo,Bw. Mnyika tayari yupo nchini humo akiwa ni mmoja wa wajumbe 12 wa Kundi la  Waangalizi wa Uchaguzi wa Jumuia ya Madola, linaloongozwa na rais wa zamani wa Nigeria Jenerali Yakubu Gowon.

Kwa mujibu wa taarifa hizo,kundi hilo lenye wajumbe kutoka nchi 12 ambao wameteuliwa kama watu binafsi liko nchini Zambia tangu Septemba 13, mwaka huu litafanya kazi hiyo hadi Septemba  27 mwaka huu.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa,uteuzi huo uliofanywa na Katibu Mkuu wa Jumuia ya Madola umetokana na  mwaliko ambao ulitolewa na Rais wa Zambia,Bw.Rupiah Banda.

Kundi hilo linajumuisha viongozi wa kisiasa, asasi za kiraia, mahakama, vyombo vya habari, taasisi za kielimu na mamlaka za usimamizi wa uchaguzi.

Kundi hilo linatarajiwa kuangalia uchaguzi wa Zambia na kutoa ripoti kama umezingatia viwango vya kimataifa vilivyowekwa na mikataba mbalimbali inayohusu demokrasia na uchaguzi, ambayo nchi hiyo imeridhia pamoja na kutoa mapendekezo ya kudumisha demokrasia katika nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment