19 September 2011

Bei ya umeme kupanda tena

*Lengo ni kuiwezesha TANESCO kujiendesha
*Pinda asisitiza bei ni lazima iongezeke
*TBL:Na sisi tutapandisha bei ya bia zetu


Grace Michael, Musoma na Mwandishi Wetu, Dar

WAZIRI MKuu, Bw. Mizengo Pinda amesema bei ya umeme inaweza kupanda wakati wowote
ili kuiwezesha serikali na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kujiendesha na kuboresha huduma zake.

Alisema hatua hiyo itafikiwa kutokana na mzigo mkubwa unaobebwa na serikali pamoja na TANESCO katika kutoa huduma hiyo ya nishati.

Bw. Pinda alitoa kauli hiyo juzi wakati akihotubia mkutano wa hadhara mjini Musoma. Katika mkutano huo Rais Kikwete aliwaeleza wananchi wa mkoani Mara kuwa tatizo la ukosefu wa umeme nchini litaendelea hadi Desemba mwaka huu na baada ya hapo litakuwa ni la kihistoria kutokana na kuwepo kwa mikakati kabambe ya kulimaliza.

Alisema hakuna cha kufanya katika suala hilo (kupanda kwa bei ya umeme) lakini aliwaondoa wasi wasi wananchi kuwa bei inaweza ikawa si kubwa.

Alisema bei iliyopo sasa itaendelea kutumika wakati hatua zingine zikiangaliwa.

“Baada ya tatizo hili la mgawo, umeme utakaokuwa unazalishwa utakuwa mwingi na wa uhakika kuliko ilivyo sasa,” alisema  Bw.Pinda na kuongeza;

“Bei ni lazima iongezeke kwani shirika la umeme linatumia dola ya Marekani senti 30 kuzalisha umeme, huku likiuza umeme huo kwa wananchi kwa dola ya Marekani senti 10, na hivyo kufanya serikali kufidia pungufu iliyopo,” alisema.

Alisema itakuwa ni vigumu kwa shirika hilo kuliachia mzigo mkubwa uliopo sasa kwa kuwa linawaeza kukwama hata kuendesha kazi zake na serikali haiwezi kuendelea kuipa TANESCO fedha kama za ununuzi wa mafuta ya kuendeshea mitambo na nyinginezo.

Alisema utegemezi wa maji katika uzalishaji wa nishati hiyo ndio uliosababisha tatizo la kuwepo kwa mgawo wa umeme baada ya mvua kuwa za wasiwasi.

Alisema mkakati wa sasa ni wa kutumia vyanzo vingine vya uzalishaji wa umeme kama kutumia makaa ya mawe, gesi asilia na upepo, vyanzo ambavyo alisema ni vya uhakika zaidi kuliko maji.

Alisema miradi kwa ajili ya upatikanaji wa umeme wa uhakika itakamilika Desemba mwaka huu na kumaliza kabisa tatizo hilo.




Naye mwandishi wetu anaripoti kuwa wakati serikali ikitangaza nia yake ya kupandisha bei ya umeme, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) imesema iwapo mgawo wa umeme nchi utaendelea na yenyewe itapandisha bei ya bidhaa zake.

Kampuni hiyo imetaka serikali kuachana na uzalishaji umeme kwa kutumia jenereta za kukodishwa na kuwekeza kwenye uzalishaji umeme kwa kutumia vyanzo asilia.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa TBL, Bw. Phocus Lasway, wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam juzi.

"Tanzania ina rasilimali nyingi za kuweza kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali asilia kama vile kwa njia ya gesi asilia
iliyogunduliwa huko Songo Songo na Mkuranga, lakini uvunaji wa njia hii haujafanywa vya kutosha," alisema, Bw. Lasway.

Alisema upatikanaji wa makaa ya mawe huko Kiwira, Nchuchuma na sehemu nyingine nchini haujaweza kutumiwa na pale ulipotumika mizengwe mingi
iliyojitokeza kama kwamba njia hii mbadala haina maana.

Bw. Lasway ametaja chanzo kingine ambacho serikali iangalie namna ya kuwekeza na kuendeleza kwa ajili ya kuzalishia umeme kuwa ni sehemu zenye upepo mkali kama vile Makambako na Singida.

TBL ilishauri  jukumu zima la uzalishaji umeme
lisiachiwe TANESCO peke yake kutokana na ukweli kwamba shirika hilo halina uwezo wa kuleta ahaueni.

“Kwanza shirika hilo limechoka, pili hawana pesa za kutosha kuendesha miradi mbalimbali na hata menejimenti imefikia kiasi kwamba inaonekana kuwa ni mzigo," alisema.

Alisema TBL inashauri serikali kuchukua hatua dhabiti ili kuhakikisha kuna mipango ya muda mfupi na mrefu wa kuhakikisha tatizo la umeme
linapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Iwapo tatizo la upatikanaji wa umeme litaendelea, Bw. Lasway alisema TBL italazimika bei za bidhaa zake kupanda uamuzi unaotokana na ongezeko
kubwa la ankara ya umeme na mafuta na kuwa mara tano zaidi ya ile ya awali kwa mwaka.

Mkurugenzi wa Ufundi wa TBL, Bw. Gavin van Wijk, alisema kuwa kampuni hiyo imeingia gharama kubwa kwa kununua jenereta na kuongeza ankara kubwa za umeme na mafuta kila mwaka.

“Kutokana na tatizo la umeme nchini, kampuni yetu imelazimika kuongeza mtaji wetu mara mbili ili kuweza kuzibeba gharama za uendeshaji bila
ya kuathiri watumiaji,” Bw. Gavin.

Alisema TBL imetumia kiasi cha dola za Kimarekani milioni 2.4 kwa ajili ya kununua jenereta kubwa la kuzalishia umeme kwa ajili ya kiwanda cha
TBL mkoani Mwanza.

Mbalina hilo, pia Gavin alisema kuwa TBL ilitumia
kiasi cha dola milioni moja kwa ajili ya manunuzi ya jenereta ya kiwanda cha TBL mkoani Arusha.

“Manunuzi ya majenerata haya ni makubwa na yanatumia mafuta mengi sana kwa saa,” alisema.

5 comments:

  1. Inashangaza sana kuona Waziri Mkuu tena MSOMI anasisitiza umeme utapanda!! Hee! hivi kuna haja gani basi ya kutumia gesi asilia na makaa ya mawe?Bei imekuwa kubwa kwa ajili ya majenereta ya kukodi tegemeo ikifika mwakani tutaanza kutumia gesi zaidi asilia toka Mtwara,songosongo na mkuranga,kabla ya mkaa wa mawe tarajio ni bei kushuka amaa kweli wabongo tutazidi kukaliwa na kulala maana hapa bei ikipanda kwa dharura hata unafuu ukija haishuki ni mbele kwa mbele hivi tuko na akili Timam kweli? mfano bei ya Sukari ktk awamu ya pili ilipanda kufikia sh.400 kisa tumeagizia toka zambia lakini kwa ahadi viwanda vyetu vikitengemaa bei itarudi ya 220 kwa kilo lakini mpk leo ni mbele kwa mbele haikurudi ni kuzidi kila kukicha na ni kwa kila bidhaa!!kweli ni vichwa vya wendawazimu tunaburuzwa kama mizoga!!

    ReplyDelete
  2. Huyu Pinda anafikiri ataendelea kuwadanganya Watanzania hadi lini?

    Tatizo kubwa la kupanda kwa nishati ya umeme ni MIKATABA YA KIFISADI iliyoingia serikali na makampuni mbalimbali kama Richmond, IPTL, nk. Kulipia capacity charges na kulipa gharama za umeme wanaoiuzia TANESCO hata kama makampuni hayo hayazalishi.

    Bila ku-address hili na kuwachukulia hatua waliotuingiza kwenye UFISADI huu umeme uataendelea kupanda hadi kiama.

    Tumechoka Pinda na majibu yako rahisi bila kushughulikia kiini cha tatizo.

    Watanzania waulizeni hawa viongozi wa CCM masuali haya magumu na wakishindwa kuyajibu wazomeeni on the spot ili wajue Tanzania ya leo sio ile ya mwaka 1947.

    Disgusted

    ReplyDelete
  3. Inashangaza sana huduma mbovu alafu wanataka kupandisha bei.Wewe unaejiita mtoto wa mkulima nafikiri umeshasahau ulikotoka,sasa unazungumza jinsi unavyojisikia madaraka tayari yameshakolea sasa uko njiani kuwa fisadi hivi karibuni.Naona hata wewe unaanza kupinda pia.

    ReplyDelete
  4. Mitambo ya kuzalishia umeme, imepatikana kifisadi; uendeshaji wake ni wa kifisadi. Tuna makaa ya mawe, jua kali, gesi na upepo wenye kasi ya kutosha. Vyanzo vya maji tunavyo vya kutosha, lakini tumewaachia wafugaji waviharibu kama bonde la mto Kilombero.
    Wananchi tupo tu na serikali yetu tunaishi kwa mtindo wa 'ili mradi kumekucha' wala hakuna mahali panapochimbika kwa upuuzi unaoendelea.
    Cha ajabu, badala ya kupambana na ufisadi ili kupunguza kabisa gharama za uendeshaji wa Tanesco, serikali inaona ni bora kuwanyonga wananchi wake, maana wananchi si wa muhimu kama walivyo mafisadi.
    Ongezeni tu hiyo bei, tutajuana mbele ya safari. Yote haya yana mwisho; Na mwisho wake uko karibu mno, ni miezi michache ijayo.

    ReplyDelete
  5. maajabu sana sasa garama zikipanda wale wanaoishi vijijin wataiona nuru kweli? mi naona nchi imewashinda bora tujue tu hamna viongozi.na bia ikipanda wenye shida tutasahauje dhiki zetu?..

    ReplyDelete