*Kikosi cha maafa chatakiwa kujiandaa
*Maeneo yatakayokumbwa nayo yatajwa
Na Stella Aron
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari juu ya kuwepo kwa
mafuriko na kukitaka Kikosi cha Maafa kujipanga kukabiliana na majanga yatakayojitokeza baada ya mvua kuanza kunyesha mwenyezi ujao.
Akizungumza Dar es Salaama jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Bi. Agnes Kijazi, alisema utabiri wa mwelekeo wa mvua kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba mwaka huu unaonesha kutakuwepo na mvua za vuli za wastani wa juu na za wastani kwa baadhi ya mikoa.
Alisema wataalam wa hali ya hewa kwa kushirikiana na wataalam wengine katika mikutano ya kutoa uchambuzi wa mwelekeo wa mvua, walibaini kuwepo kwa ongezeko la mvua na athari zake.
"Katika mikutano hiyo ilitathminiwa kuwa kutakuwa mvua kwenye eneo la Ukanda wa Pembe ya Afrika na Kusini mwa Afrika ambapo viashiria vikuu ni pamoja na hali ya joto ya bahari katika maeneo ya Bahari ya Hindi, tropikali ya bahari ya Pasifiki na Atlantiki, " alisema B. Kijazi.
Alisema katika mwelekeo wa mvua kwa kipindi cha miezi hiyo mitatu maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka, yaani Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Pwani ya Kaskazini na maeneo ya Kanda ya Ziwa Victoria mvua zinatarajiwa kuwa juu ya wastani.
Pia alisema mvua katika maeneo ya Kaskazini mwa nchi zinatarajia kuanza kunyesha wiki ya pili ya mwezi huu na kusambaa katika maeneo mengine yanayopata mvua kwa misimu miwili kwa mwaka.
Kwa upande wa ukanda ya Ziwa Victoria, mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza Shinyanga na Kigoma Kaskazini, mvua zinatarajiwa kuanza kunyesha wiki ya pili ambapo zitakuwa mvua za juu ya wastani katika maeneo mengi.
Mkurugenzi huyo alisema ukanda wa Pwani Kaskazini yaani mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Morogoro Kaskazini na Mashariki, Visiwa vya Unguja na Pemba mvua zinatarajia kuanza wiki ya pili ya mwezi ujao na zinatarajia kuwa juu ya wastani katika maeneo mengi.
Mikoa mingine ambayo inatarajia kuwa na mvua za wastani wa juu ni mikoa ya Singida na Dodoma ambapo mikoa ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki yaani mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara inatarajia kuwa za wastani na juu ya wastani.
Alisema Kanda ya Magharibi yaani mikoa ya Tabora, Rukwa na Kigoma mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya tatu na ya nne ya Novemba na zinatarajia kuwa za wastani hadi wastani wa juu.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo, TMA inatoa tahadhari kwa mamlaka mbalimbali ikiwemo kikosi cha majanga kujiandaa kwenye vituo vya kitaifa ili kukabiliana na hali hiyo.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa kutokana na utabiri huo wamekishauri kikosi hicho kuchukua tahadhari mapema ili kukabiliana na athari zitokazo na mvua hizo kwa maeneo ambayo yanatarajiwa kupata mvua juu ya wastani.
"Mvua hizo zina uwezekano wa kusababisha mafuriko, mmomonyoko wa ardhi na uharibifu wa miundombinu ambapo maeneo mengine yatakayopata mvua chini ya wastani ya uwezekano mkubwa wa kupata uhaba wa chakula, " alisema.
Pia mkurugenzi huyo TMA alitoa tahadhari kwa Wizara ya Nishati na Madini kuzingatia usimamizi mzuri wa matumizi ya maji pamoja na mbinu za kuvuna maji ya mvua kenye mabwawa.
"Kuna uwezekano wa mabwa yaliyoko kwenda ukanda ambao mvua zitanyesha nyingi kupata maji ingawa hayataweza kujaa hivyo wizara husika haina budi kusimamia kwa uangalifu suala hili," alisema.
Aidha alisema kutokana na mvua hizo kuna uwezekano pia wa kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko yanayotokana na hali ya hewa hivyo Wizara ya Afya na kushauri Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kujipanga.
Hata hivyo alisema hali ya malisho inatarajia kuimarika katika maeneo mengi ya nchi. Hata hivyo aliwashauri wafugaji kuzingatia ushauri kutoka kwa maafisa mifugo ambapo upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo na shughuli za kiuchumi inatarajia kutosheleza.
Aidha alisema TMA itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa za mwelekeo wa mvua nchini.
No comments:
Post a Comment