Na Faida Muyomba, Geita
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Bw.Joseph Msukuma, ametangaza kujivua nyadhifa zake zote ndani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) ikiwa ni
muda mfupi tu baada ya madiwani kumuondoa katika nafasi hiyo.
Aidha kabla ya kuanza kwa kikao hicho, Mbunge wa jimbo la Nyangh'wale, Bw.Hussein Kasu, alitoleana maneno makali na Ofisa mmoja wa polisi, mrakibu H.A.Balige,baada ya kumzuia katibu wa mbunge huyo kuingia ndani ya ukumbi wa Halmashauri uliokuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi kuepusha fujo kutokea.
Nafasi alizokuwa nazo ni pamoja na umakamu mwenyekiti wa ALAT mkoa wa Mwanza na ile ya udiwani wa kata ya Nzera iliyomwezesha kushika wadhifa huo wa kuiongoza Halmashauri hiyo.
Uamzi huo umekuja baada ya kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani kufanyika jana na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Bw. Abbas Kandoro, kikiwa na ajenda moja ya kumjadili mwenyekiti huyo.
Kikao hicho kilianza saa 4.55 chini ya Makamu Mwenyekiti Bw. Christopher Kadeo, ambapo Mkuu wa Mkoa alitoa mwongozo ikiwa ni pamoja na kuwataka madiwani kumpa nafasi mtuhumiwa kujibu hoja zake nna kuwa baada ya hapo zitapigwa kura kwa mjibu wa sheria.
Alisema,katika kikao hicho,aliwataka madiwani kuwa huru katika maamuzi yao ambayo yatakuwa na lengo la kuwaletea wananchi wa wilaya ya Geita maendeleo na si vinginevyo. Baada ya hapo madiwani walikaa kama kamati na baadaye zilipigwa kura kwa ajili ya kutoa uamuzi .
Akitangaza matokeo ya kura hizo,Mwenyekiti wa kikao hicho, alitangaza kuwa kura zilizopigwa ni 64,ambapo zilizoafiki kuondolewa ni 45,zilizokataa 13 huku 13 zikiharibika.
Mara baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo,Bw.Msukuma aliomba nafasi ya kushukuru wapiga kura wake na ndipo alitangaza kujivua madaraka nafasi zake zote ndani ya CCM.
Tuhuma alizokuwa akikabiliwa Mwenyekiti huyo ni pamoja na matumizi mabaya ya uongozi,nidhamu pamoja na kushindwa kazi ambapo kikao hicho ni cha pili baada ya kile cha kwanza kilichofanyika Agosti,17 kuvunjika kutokana na kutokamilika kwa taratibu kwa mujibu wa sheria.
No comments:
Post a Comment