Na Zahoro Mlanzi
MREMBO Rose Albert amewabwaga washiriki wenzake na kutwaa taji la Vodacom Miss Talent 2011 katika shindano la siku ya kuonesha vipaji lililofanyika kwenye hotel ya
Giraffe iliyopo Mbezi, Dar es Salaam.
Katika siku hiyo ya vipaji, warembo wanaowania taji la Vodacom Miss Tanzania 2011 walichuana vikali vipaji mbalimbali vikiwemo kuimba, kucheza muziki wa kizazi kipya 'Bongo flava, nyimbo za kiutamaduni na maigizo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, ilieleza kwamba Meneja Uhusiano na Habari za Mtandao, Matina Nkurlu alisema lengo la siku hiyo ni kutaka kutambua vipaji walivyonavyo warembo hao wakiwa tayari kwenda kwenye hatua ya mwisho ya shindano hilo litakalofanyika Mlimani City, Septemba 10, mwaka huu.
Alisema mbali ya kutaka kujua vipaji vyao pia imesaidia kuibua vipaji vya warembo hao mbali na fani ya urembo wanayojihusisha nayo.
“Tukiwa kwenye siku ya Vodacom Miss Talent warembo wameonesha vipaji vyao vya kipekee jambo lililowafanya pia kuendelea kuwa pamoja kama ilivyo tasnia hiyo kwamba inawaunganisha watu wote bila kujali dini rangi au kabila," alisema Nkurlu.
Naye mrembo Rose aliyetwaa taji hilo, alisema siku hiyo ni ya faida kwake kwani ameweza kuonyesha vipaji vyake mbalimbali alivyonavyo na kujifunza mengi toka kwa washiriki wenzake.
Alisema mbali ya kuonesha vipaji vyake, pia amepanua mtazamo wa kiakili kwani ni moja ya fani zinazoenda kushindaniwa katika shindano la Miss World kwa atakayebahatika kuliwakilisha Taifa letu.
“Vipaji ni moja ya vipengele kwenye shindano la urembo la dunia, hivyo kwa atakayebahatika atafanya vizuri kwani vipaji ni kitu muhimu tayari kwa kwenda kushiriki michuano hiyo ya urembo ya dunia.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Itifaki wa Kamati ya Vodacom Miss Tanzania, Albert Makoye alisema ari waliyonayo warembo inaonesha utayari wao katika kuliwakilisha taifa katika medani za kimataifa.
Aliwaomba watanzania waendelee kuwapigia kura washiriki hao wanaoishi ndani ya jumba la Vodacom na watazame vituo vya televisheni vinavyoonesha shindano hilo.
No comments:
Post a Comment