Na Peter Mwenda, Igunga
CHAMA cha Wananchi (CUF) jana kilizindua kampeni zake kwa kishindo jimboni Igunga huku Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba akiwataka wananchi kutomchagua
mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Kafumu Dalaly kwa madai kuwa mikataba mibovu ya madini iliingiwa wakati mgombea huyo akiwa kamishna huku Bw. Benjamin Mkapa akiwa mkuu wa nchi.
Katika uzinduzi huo uliofanyika akizindua kwenye uwanja wa Sokoine ulioko katikati ya mji wa Igunga na kuhudhuriwa na umati wa watu, Prof. Lipumba alidai mgombea wa CCM alishirikiana na Bw. Mkapa kuingia
mikataba ya kifisadi.
Aliitaja mikataba hiyo kuwa ni wa mgodi wa Kiwira, Meremeta, North Mara na mingineyo ambayo imesababisha wananchi wa maeneo husika kufukuzwa na kutothaminiwa.
Alimtaka Bw. Mkapa kuepuka aibu ya kuwadanganya wananchi wa Jimbo la Igunga na Tanzania kuwa ndiye aliyeleta maendeleo na mabadiliko katika kipindi chake cha miaka kumi aliyokuwa madarakani.
Alisema kuwa mkataba wa IPTL Bw. Mkapa alihusika kuusaini ambapo mamilioni ya fedha zilikwapiliwa na kuacha wananchi wakiteseka mpaka leo na kuongeza kwamba pia ununuzi wa rada ulikuwa wa udandanyifu na uisiozingatia maslahi ya Watanzania.
Alidai baada ya kuhodhi migodi na vitu vingine tena Rais Jakaya Kikwete ameendeleza mikakati iliyoachwa
bila kutekelezwa huku akiweka marafiki wake katika nafasi nyeti ambazo zimewashinda kuongoza.
Prof. Lipumba alisema kuwa Jimbo la Igunga linahitaji mabadiliko ya uongozi ngazi ya ubunge kwa kuwa limekuwa likishikiliwa na mmoja wa wanasiasa anayetuhumiwa kwa ufisadi akishirikiana na viongozi ngazi za juu na kushindwa kuwatetea wananchi huku wakikosa huduma muhimu kama maji, barabara, afya na elimu.
Alisema kuwa CCM ilipewa ridhaa ya kuwaongoza wananchi kwa miaka 50 lakini mpaka sasa vijana zaidi ya milioni 21 hawana ajira na baadhi ya viwanda vimekufa na kusababisha uzalishaji kupungua ndani ya nchi huku serikali
ikitegemnea bidhaa kutoka nje ya nchi.
Awali mwenyekiti huyo wa CUF alipokelewa eneo la Hani Hani kilomita 2.8 kutoka Igunga mjini akikokotwa na punda ambapo alizungushwa mitaa mbalimbali ya jimbo hilo akifuatana na mgombea wa CUF Bw. Leopold Mahona kabla ya kuingia Uwanja wa Sokoine kuhutubia.
Naye Bw. Mahona alijinadi kwa wananchi hao kwa kuomba kumuchagua ili kuwaondolea matatizo yanayowakabili ikiwemo maji, barabara, huduma za afya, elimu pamoja na kuwajengea daraja la Mbutu ndani ya siku 400.
Alisema kuwa ikiwa atachaguliwa atakuja na sera za Nishati, Kilimo na Jamii (NIKIJA) na kuanzisha vikundi vidogovidogo (Saccos) vya wajasiriamali kwa wanawake katika tarafa nne za Jimbo la Igunga.
Mwenyekiti wa TLP Bw. Moses Mkongwe aliwaomba wananchi hao wamchague Bw. Mahona kwa sababu ana kila sifa na anajua shida za wananchi ana uwezo wa kuzitatua.
No comments:
Post a Comment