Na Zahoro Mlanzi
LIGI Kuu ya Tanzania Bara, inaendelea tena leo kati ya Polisi Dodoma itakayokaribisha Mtibwa Sugar ya Morogoro na JKT Ruvu itaumana na Moro United katika michezo
itakayopigwa Dodoma na Dar es Salaam.
Polisi ambayo ipo nafasi ya saba katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi sita itashuka uwanjani na matumaini ya kuibuka na ushindi, baada ya mchezo wake wa mwisho dhidi ya Moro United ambapo iliibuka na ushindi wa mabao 5-2 ukiwa pia ndiyo ushindi wao wa kwanza katika ligi hiyo.
Mtibwa yenyewe itakuwa na kazi moja ya kuhakikisha inaendeleza wimbi lake la ushindi, baada ya mchezo wa mwisho dhidi ya Villa Squad kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 na kufikisha pointi 11, ikiwa katika nafasi ya tatu sawa na Azam (kabla ya mchezo wa jana) ikitofautiana kwa mabao.
Kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam wenyeji JKT Ruvu wataumana na Moro United, ambayo itaingia uwanjani ikiwa imejeruhiwa kutokana na kupokea kichapo cha mabao 5-2 na Polisi, hivyo itataka kurekebisha makosa hayo.
JKT yenyewe itashuka uwanjani kwa matarajio ya kushinda mchezo huo, kutokana na mechi iliyopita ambapo ilicheza na Toto African ya Mwanza na kugawana pointi, na kufikisha pointi nane katika ikiwa nafasi ya nne.
Mashabiki wengi wa soka nchini macho na masikio yatakuwepo mkoani Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri, ambapo wenyeji Polisi watakuwa na kazi kubwa kuhakikisha inaifunga Mtibwa kwani ushindi mnono walioupata ndiyo kivutio kikubwa cha watu kuwa na kiu cha kuona kitakachotokea.
No comments:
Post a Comment