22 September 2011

Wabunge wa Norway watakiwa kuyabana makampuni ya kigeni

Na Tumaini Makene

WABUNGE wa Tanzania wamewaomba wenzao wa Norway, kujenga ushawishi kwa nchi za Magharibi ili kwa namna ile ile zinavyopambana kuwang'oa viongozi wabaya
madarakani katika Bara la Afrika, basi pia ziyakabe koo makampuni makubwa ya kimataifa ambayo yanaingia mikataba ya kinyonyaji na serikali za bara hili, ikiwemo Tanzania.

Walisema kuwa kama ilivyo kwa viongozi wabaya, mikataba hiyo ya uwekezaji, mathalani katika uchimbaji wa madini, nayo imeendelea kuwa moja ya vikwazo vya maendeleo ya nchi hizo, ambapo imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa serikali kushindwa kutoa huduma za jamii, kama vile afya bora, elimu na nyinginezo.

Hayo yalisemwa jana na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Bw. Mussa Zungu, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kubadilishana mawazo kati ya wabunge wa Tanzania na wajumbe wa kamati ya aina hiyo kutoka Bunge la Norway.

"Tumezungumzia masuala ya Libya, ambapo msimamo wetu ni ule ule wa serikali...katika hili Afrika haikutendewa haki, Umoja wa Afrika (AU) uliachwa pembeni, haukupewa nafasi katika maamuzi ya kusuluhisha mgogoro wa Libya.

Pia tumewaambia watusaidie kutokana na uzoefu wao katika uchimbaji wa madini...mafuta ambapo wamekuwa na mafanikio," alisema Bw. Zungu, ambaye pia ni Mbunge wa Ilala.

Mbunge wa Viti Maalum, Bi. Angela Kairuki aliwaomba wabunge hao kuendelea kujenga mahusiano na wabunge wa Tanzania, huku akitoa rai kwao kwao kusaidia nchi kutokana na uzoefu juu ya masuala ya utungaji wa katiba na uwakilishi sawa wa 50 kwa 50, wanaume kwa wanawake katia vyombo vya maamuzi.

Katika kikao cha wabunge hao wa Norway na Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wabunge wa Tanzania walisema kuwa nchi bado inakabiliwa na changamoto za utaalam na teknolojia katika baadhi ya maeneo muhimu kwa ajili ya maendeleo.

Mbunge wa Mbozi Magharibi, Bw. David Silinde alisema kwa muda mrefu nchi ilikuwa ikitegemea umeme unaozalishwa kwa nguvu za maji, lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababisha mvua kutotabirika na kuongezeka kwa mahitaji ya nishati hiyo.

1 comment:

  1. Kwani hao viongozi wabaya wa Africa wanashikiwa bunduki? Na je, kwani hao viongozi mafisadi wa kiafrika wanachukua madaraka kwa nguvu au wanachaguliwa na wananchi wao wenyewe na kupigiwa madebe na wabunge wake? Ni lini hata siku moja bunge la kiafrika limepiga kura ya kutokuwa na imani na raisi wake ambaye ni fisadi? Mbona wabunge wa Tanzania wamekalia mikia yao wakati wanawajua waliohusika na mikataba mibovu ni nani, na walioiba mabilioni na kuyaficha nchi za kibepari ni nani? Wabunge wamechukua hatua gani wakashindwa ndipo waanze kuomba misaada kutoka Norway. aidha wabunge hao ni wanafiki, mambumbumbu, au matahira - au pengine vyote vitatu.

    ReplyDelete