21 September 2011

Kesi ya madiwani CHADEMA yafutwa

Na Queen Lema, Arusha 

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha imetupilia mbali kesi iliyofunguliwa na madiwani watano waliofukuzwa uanachama na Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) na kuamriwa kulipa gharama za kesi hiyo.

Madiwani hao waliwasilisha pingamizi la kufukuzwa uanachama kwa maelezo kuwa hawakutendewa haki na uongozi wa CHADEMA.

Uamuzi wa kutupilia mbali madai ya madiwani hao ilitolewa mahakama hapo jana na Hakimu Mkazi wa Arusha Hawa Mguruta baada ya kupitia hoja nne za pingamizi zilizowasilishwa mahakamani hapo.

Hoja za madiwani hao ziliwasilishwa na wakili wao, Bw. Severine Lawena huku mawakili wawili, Bw. Method Kimomogoro na Albert Msando wakitetea CHADEMA.

Katika shauri hilo la madai namba 17 la mwaka huu, washtakiwa walikuwa ni CHADEMA na Bw. Freeman Mbowe binafsi, huku wadai wakiwa ni madiwani watano waliofukuzwa kwenye chama hicho.

Madiwani hao kata zao kwenye mabano ni Naibu Meya wa Manispaa ya Arusha Bw. Estomii Mallah (Kimandolu), Bw. John Bayo (Elerai), Bw. Ruben Ngowi (Themi), Bi. Rehema Mohamed (Viti Maalumu) na Bw. Charles Mpanda (Kaloleni).

Hakimu Mguruta alisema anakubaliana na hoja za mawakili wa walalamikiwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kuchunguza maamuzi ya chombo binafsi kama ilivyo Kamati Kuu ya CHADEMA.

Alisema chombo chenye mamlaka hayo ni Mahakama Kuu ya Tanzania.

"Nakubaliana na hoja kuwa CHADEMA haiwezi kushtakiwa kwa jina lake, jina hilo halina uhai kisheria hivyo haiwezi kushtaki wala kushtakiwa kwa mujibu wa sheria," alieleza Hakimu Mguruta.

Alisema anakubaliana na hoja ya mawakili hao kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho (Bw. Mbowe) hawezi kushtakiwa binafsi na kwamba alipaswa kushtakiwa kwa nafasi yake au Uenyekiti wa Taifa vinginevyo hataweza kutekeleza maelekezo ya mahakama hiyo ndani ya CHADEMA.

“Mbowe alipaswa kushtakiwa kwa nafasi yake ya uenyekiti wa Taifa kwani endapo ataondolewa kwenye nafasi hiyo au kujiuzulu hataweza kutekeleza maamuzi ya mahakama wala kuendesha na kusimamia maamuzi ya vikao ndani ya CHADEMA,” alisema hakimu mguruta.

Alisema kesi hiyo imefika mahakamani hapo ikiwa imepitwa na wakati kwa kuwa tayari madiwani hao walishakata rufaa kwenye Baraza Kuu la CHADEMA.

Baada ya hukumu hiyo wanachama wa chama hicho waliondoka mahakamani hapo kwa maandamano na mbunge wa Arusha mjini Bw. Godbless lema.

No comments:

Post a Comment