Na Agnes Mwaijega
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeendelea kushusha bei za bidhaa za petroli, ambapo safari hii mafuta ya petroli kwa Dar es Salaam
yatakuwa yakiuzwa kwa sh. 2,031 katika kipindi cha wiki mbili zijazo yakiwa yameshuka kutoka sh. 2,070.
Akizungumzia kushuka kwa bei ya mafuta, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Bw. Titus Kaguo, alisema bei ya mafuta ya dizeli kwa Dar es Salaam itakuwa ni sh. 1,954 ikiwa imeshuka kutoka sh. 1,999 na mafuta ya taa itakuwa ni sh. 1,933 ikiwa imeshuka kutoka sh. 1,980 bei iliyokuwa ikitumika hadi Jumapili ya jana.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bw. Kaguo, kushuka kwa bei za leo ni mfululizo wa kushuka kwa bei tangu kuanza kwa matumizi ya kanuni mpya iliyoanza rasmi Agosti 1, 2011.
“Bei za rejareja kwa aina zote za mafuta zimeshuka ikilinganishwa na bei zilizoanza kutumika kuanzia Agosti 29 2011. Bei hizi zimeshuka kwa viwango mbalimbali ambapo petroli imeshuka kwa sh. 38.03 sawa na asilimia 1.84, dizeli sh. 45.15 sawa na asilimia 2.26 na mafuta ya taa bei zimeshuka kwa sh. 46.15 sawa na asilimia 2.33.”
Bw. Kaguo alisema mabadiliko ya bei yametokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia ambapo petroli imeshuka kwa asilimia 2.54, dizeli asilimia 3.78 na mafuta ya taa kwa asilimia 3.50.
Hata hivyo, Bw. Kaguo alisema bei za mafuta katika soko la ndani zingeshuka zaidi kama shilingi ya Tanzania isingeendelea kushuka thamani dhidi ya dola ya Marekani.
Bw. Kaguo alisema katika kipindi hicho, thamani ya shilingi ya Tanzania imeshuka kwa asilimia 0.20 ikilinganishwa na dola ya Marekani.
Akizungumzia faida ya matumizi ya kanuni mpya, Bw. Kaguo alisema bei za rejareja zingepanda zaidi endapo kanuni ya zamani ingeendelea kutumika.
No comments:
Post a Comment