Na Eliasa Ally, Iringa
MKURUGENZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini, Bi. Tina Sekambo, amewataka wananchi wilayani humo kupanda miti ya matunda na kivuli katika msimu wa
mvua.
Bi. Sekambo aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Majira ju ya umuhimu wa kupanda miti ya matunda na mingine ili kukabiliana na majanga mbalimbali yanayotokana na mmomonyoko wa ardhi na kutunza mazingira.
Alisema watu wengi hawana utamaduni wa kupanda miti hadi wahamasishwe na Serikali hivyo kila mtu anapaswa kuweka mkakati binafsi wa kupanda miti kila mwaka.
Aliongeza kuwa, miti ya matunda ina faida kubwa kwa uhifadhi wa mazingira na kulinda afya za familia.
“Watu wengi hawafahamu umuhimu wa miti, miti ya matunda ina faida kutokana na familia nyingi kutumia matunda yake, kuzuia mmomonyoko na kutunza mazingira,” alisema.
Alisema Halmashauri ya Iringa, matunda yameonekana kupandwa na Misheni za Kanisa Katoliki eneo la Tosamaganga lakini wananchi hawajaonesha mwamuko wa kupanda miti ya matunda.
Aliongeza kuwa, Watanzania wanapaswa kujifunza kwa raia wa nchi jirani za Malawi, Kenya na Uganda ambao wanazingatia suala la upandaji miti ya matunda na mingine ambayo inawaletea manufaa makubwa na kukuza kipato chao.
No comments:
Post a Comment