20 September 2011

CUF yakerwa kuitwa CCM-B

*Wabunge sita watua Igunga kuongeza nguvu

Na Peter Mwenda, Igunga

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimekionya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuacha mara moja kutangaza
kudanganya wananchi wa Jimbo la Igunga kuwa chama hicho kisipewe kura kwa madai kuwa ni CCM-B.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni ya uchaguzi mdogo Jimbo la Igunga juzi, Kaimu Katibu Mkuu wa CUF-Bara, Bw. Julius Mtatizo alisema CHADEMA imekuwa ikiwadanganya wananchi kuwa CUF ni CCM-B, wasikichague kwa sababu hakitaleta maendeleo jambo ambalo ni udanganyifu ambao unastahili adhabu.

Alisema CUF imevumilia sana kauli hizo na sasa imefika kikomo, hivyo kilichobaki ni wao kuweka hadharani mabaya ya CHADEMA kwa sababu ya upotoshaji huo kwa wapiga kura wa Igunga.

Bw. Mtatiro alisema cha kushangaza, ni kwa nini CHADEMA iseme uongo wakati CUF haijawahi kusema mtindo wa uongozi wa upendeleo uliopo katika chama hicho, ambao hauna tofauti na yale yanayofanywa na chama tawala CCM.

"Mfumo wa uongozi wa CHADEMA hauna tofauti na ule wa CCM kwa sababu ule mfumo wa uongozi wa kupeana ulipo CCM ambao hautawahi kutokea CUF," alisema Bw. Mtatiro.

Alisema CHADEMA ilipata viti maalumu 36 na kushindwa kugawa kwa kuzingatia uwakilishi wa wananchi, bali walipendeleana wao kwa wao kwa kugawa viti 16 kwa mkoa wa Kilimanjaro pekee ambako viongozi wa chama hicho, walitoa kwa wake zao, wadogo zao na jamaa zao.

Alisema CUF Tanzania bara na Zanzibar walipata viti maalum kumi ambavyo ilivigawa bila upendeleo Dodoma (Bi. Moza Abeid), Mwanza (Bi. Mkiwa Kimwanga , Tanga Bi, Amina Mwidau, Mtwara (Bi. Clara Mwatuka, Kaskazini Pemba (Bi. Riziki Omar Juma), Mjini Magharibi Bi. Amina Amour na Kusini Magharibi (Bi. Thuwaiba Idris) ambao wanakilisha wa wananchi badala ya kulimbikizia kundi chache.

Alisema suala la Serikali ya Umoja Zanzibar ni mfumo uliofikiwa na Wazinzibari wenyewe ili kuondoa uhasama uliokuwepo, sasa inakuaje CHADEMA iseme CUF imeingia mkataba wa urafiki na CCM.

Wabunge waongeza nguvu

Wabunge sita wa CUF kutoka Zanzibar waliokuwa katika msiba wa meli ya M.V Spice Islanders wamewasili Igunga kuanza kampeni za kumnadi mgombea wa chama hicho, Bw. Leopold Mahona.

Wakitambulishwa katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Nanga juzi jioni, Kaimu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Bw. Julius Mtatiro alisema pamoja kuwa msiba huo ni mkubwa na umegusa familia za wabunge hao, wamekuja kuongeza nguvu kuhakikisha chama hicho kinachukua kiti.

Waliotambulishwa ni Mbunge wa Nungwi ambako meli hiyo ilizama, Bw. Yusuf Haji Khamis, Bw. Rashid Ali Omar (Kojani), Mohamed Habib Mnyaa (Mkanyageni), Haroub Mohamed Shamis (Chonga), Bw. Salim Hemed Khamis (Chambani).

Katika mkutano huo mgombea ubunge wa CUF, Bw. Leopold Mahona alisema akichaguliwa atahakikisha wananchi wa Kata hiyo wataondokewa na kero zinazowasumbua kwa miaka mingi bila kupatiwa ufumbuzi.

4 comments:

  1. Hivi hakuna uwezekano wa TBC1, StarTV, ITV etc kuandaa mdahalo wa wazi kwa wagombea hawa Dr. Kafumu (CCM), Bwn Kashindye (CDM) na Bwn. Mahona (CUF) ili wana Igunga tujue pumba ni zipi na mchele ni upi?

    Haijalishi hata kama Kafumu (CCM) ataingia mitini kama ilivyo ada ya CCM, kwani hilo litakuwa ni bao la kisigino kwa CDM na CUF.

    Jamani wana Igunga tunaomba mdahalo wa wagombea hawa watatu.

    ReplyDelete
  2. mdahalo hauna maana inatakiwa igunga wipe chadema tuuuuuu

    ReplyDelete
  3. Vyama vya upinzani lazima wajenge umoja ili kuiondoa CCM madarakani,CCM inatupeleka pabaya,siasa za ushindani zitakuwa za maana na tija kwa taifa pale ambapo budget za serikali zisizo na tija hazitapitishwa,itawezekana endapo 60% ya wabunge watatoka upinzani.Chadema lazima wajitazame upya,wasijione kuwa wao ni bora kuliko wenzao wa upinzani,mtazamo huo hautakisaidia chama hicho na kamwe wasitegemee kushika madaraka ya uraisi.Waache ubabe,kujiona wao ni bora,lazima waanze mchakato wa kutafuta kuungwa mkono na wenzao wa CUF chama ambacho ni kikomavu na makini kwa mtazamo wa wengi werevu.Angalia wenzetu wa Kenya,waliungana wakaitoa Kanu madarakani,hali ya maisha kwa wananchi imebadilika kulinganisha na kwetu Tanzania.Kamwe ubinasfi hautatusaidia,angalia ubinafsi ndani ya CCM unavyoingamiza nchi,maisha ni magumu kwa sehemu kubwa ya Watanzania.NI NDOTO KUISHINDA CCM IGUNGA KWA STYLE HII YA CUF NA CHADEMA KUSHUTUMIANA.

    BY:Mlimbwa 0713 046466

    ReplyDelete
  4. Mlimbwa unasema kweli. chadema wasijidanganye kwamba wataiweza ccm bila kuungwa mkono na vyama vingine vya upinzani

    Inabidi chadema wajiangalie upya, waache ubabe, waache kuvisengenya vyama vingine vya upinzani. chadema isidhani itashinda kiti cha ubunge wa Igunga kwa kuvishambulia vyama vyote.Mbona vyama vingine vya upinzani havikishambulii chadema?

    ReplyDelete