24 August 2011

Yatima 7,000 wapewa msaada Na Salim Nyomolelo

KIKUNDI cha Ushauri na Taarifa cha Upendo kimetoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto yatima 7,000 wenye umri kati ya miaka sita hadi 12 wanaoishi mkoa wa
Dar es Salaam na Pwani jana.

Akizungumza na gazeti hili mkurugenzi wa kikundi hicho Bi.Wandoa Mwabu, alisema huo umetolewa ili kusaidia watoto hao.

Kila mtoto alipewa godoro la kulalia,daftari za shule nne,vitambaa vya sare za shule,khanga doti moja,kandambili,shuka na kalamu.

Alisema kati ya watoto waliopewa msaada huo 3,500 wanatokea maeneo ya Mkoa wa Pwani na 3,500 wanatokea Dar es Salaam.

Alisema ili mtoto aweze kupata msaada huo ni lazima afike na mlezi wake na baada ya kukabidhiwa anapigwa picha akiwa na vifaa alivyopewa kwa ajili kumbukumbu.

Aliongeza kuwa walifanya jitihada za kutembelea katika shule za msingi kwenye mikoa hiyo ili kupata taarifa na majina ya watoto wanaostahili kupata vifaa hivyo, ambavyo vitawasaidika katika masomo yao.

"Tumechukua watoto yatima wenye umri kati ya miaka sita hadi 12 wa shule za msingi ili kuwapunguzia gharama walezi, kwani wana majukumu mengine pia,"alisema Bi.Mwabu

Hata hivyo alisema wataangalia uwezekano wa kuwasaidia yatima wengine katika baadhi ya mikoa iliyobaki awamu inayofuata ambayo bado hawajapanga itafanyika lini na wapi.

No comments:

Post a Comment