24 August 2011

CCM yakiri watumishi kuvujisha siri nyeti

Na Peter Mwenda

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimekiri kuwa kuna baadhi ya watumishi wa umma ambao si waaminifu wanaovujisha siri za Serikali.Akizungumza katika mahafali ya
23 ya Chuo cha Biashara na Uhazili cha Splendid, Dar es Salaam juzi Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Kilumbe Ng'enda, alisema makatibu muhtasi ni wanataaluma na wenye maadili ya kutunza siri za ofisi, hivyo hakuna sababu ya kuwakumbatia wasiofuata maadili.

Alisema ni kweli risala ya wanachuo 98 waliohitimu katika chuo hicho wamesema kweli kuwa wafanyakazi wa serikali wengi wanavujisha siri, hivyo CCM inaahidi kuwaondoa na kuweka wenye maadili ya taaluma zao.

Bw. Ng'enda alisema wapinzani wamekuwa wakitumia visingizio vya maandamano kupinga Serikali ya CCM, lakini wajue kuwa hiyo si njia ya kutatua kero za wananchi.

Aliwataka wapinzani kutekeleza ahadi zao kwa wananchi badala ya kutafuta visingizio.

Alisema CCM imejipanga kushinda Jimbo la Igunga na lazima italichukua kwa sababu wananchi wanapenda chama hicho kwa sababu ndicho kinawakomboa katika matatizo mbalimbali ya elimu, uchumi na kuendelea kuwajengea amani.

Bw. Kilumbe aliahidi kuwatafutia ajira wahitimu hao katika ofisi za chama ngazi ya wilaya za Ilala, Kinondoni na Temeke na kutoa kompyuta mbili na mashine za kupiga chapa  mbili kwa ajili ya chuo hicho.

Awali Mkuu wa Chuo hicho, Bw. Caasim Taalib, alisema chuo hicho kinatoa nafasi kumi kwa vijana wa CCM kusoma bure kozi ya uhazili katika chuo hicho na kati ya wahitimu hao 65, wamekubali kujiunga na CCM na kuacha vyama vyao vya upinzani.

1 comment:

  1. Bwana Ng'enda ni wazi kuwa umepotoka kabisa. ujue wazi kuwa wanachokifanya watumishi waaminifu ni kuibua mambo maovu yanayofanywa na viongozi ili wenye mali (WANANCHI) ambao pia ni waajiri wa viongozi wajue kinachoendelea kisha waangakie hatua za kuchukua. uovu kamwe hauwezi kuwa siri. serikali inayoficha uovu na kuuita siri, inakuwa imepoteza uhalali wa utumishi kwa Wananchi. Itatumikiaje Wananchi huku ikiwalinda wahalifu wanaohujumu na kuteketeza mali na haki za Wananchi haohao? Ndugu yangu, maovu yanafichuliwa bila kujali na anayafanya. serikali haiwezi kusimamia uadilifu wakati siyo adilifu.
    Jamani mmeng'ang'ania kuwa maandamano hayajengi; Sasa mnataka kutuambia kuwa taifa hili litajengwa kwa tabia hii ya viongozi kuendekeza wizi, ufisadi na ujambazi dhidi ya raia? Hivi kwa nini wewe Bwana Ng'enda na wenzako mnapoteza nguvu nyingi kukemea maandamano badala ya kukemea uovu wa serikali? Hivi mnajua ni Wananchi wangapi wanakufa kutokana na madhara ya ufisadi? njaa, Ukosefu wa madawa, madawa feki, vitu feki, rushwa kwenye leseni za udereva n.k. Ujue kuwa vyote hivi vinateketeza maisha ya Watanzania kwa asilimia zaidi ya sitini nchini Tanzania. Sasa ni gaidi yupi anayeua watu wengi namna hii hapa duniani.
    Wanachi wanaandamana kupinga taifa lao kuangamia, ninyi mnapinga maandamano, ina maana mnafurahia kuona tukiangamia? kwa nini mmekuwa vipofu kiasi hiki? au kwa vile wanaofanya ufisadi ni wenzenu na hivyo ni lazima muwalinde? Halafu mnajidanganya kuwa wananchi tunawapenda. Ninyi kabisa! labda tume ya uchaguzi.

    ReplyDelete