17 August 2011

Yanga yatishia kugomea mechi

*Waitaka TFF kuwalipa deni leo

Na Zahoro Mlanzi

'UKIMWAGA mboga, nasi tunamwaga ugali', ndivyo unavyoweza kuzungumza kutokana na uongozi wa Yanga kulitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuilipa
deni lake la sh. milioni 18.6 mpaka kufikia leo saa 5 asubuhi, vinginevyo hawataingiza timu katika mchezo wa leo dhidi ya Simba.

Miamba hiyo ya soka nchini inatarajiwa kuumana leo katika mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa saa mbili usiku Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mchezo maalumu kwa ajili ya ufunguzi wa Ligi Kuu Bara itakayoanza Jumamosi.

Mbali na hilo, tayari klabu hizo kila moja imelamba sh. milioni 84 baada mechi hiyo kuuzwa kwa Kampuni ya Big Born, kilichobaki ni timu hizo kuoneshana kazi.

Akizungumza Makao Makuu ya klabu hiyo Mitaa ya Jangwani na Twiga, Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu,,  alisema TFF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania) limekiuka makubaliano waliyoingia wakati wanafanya kikao cha mchezo huo.

"Kiukweli tayari Big Born ilitoa mgawo wetu kwa ajili ya mchezo huo na kila timu imepata sh. milioni 84 na asilimia 15 za fedha zilizotolewa na kampuni hiyo zimekwenda TFF," alisema Sendeu na kuongeza;

"Lakini wakati tunajadili tulikubaliana na TFF kwamba, watatulipa fedha zetu za zawadi za Berko (Yaw) sh. milioni mbili na fedha nyingine tunazowadai,  ambapo ni sh. milioni 16, katika fedha watakazopata, hivyo tunajua fedha wanazo tunachotaka watulipe," alisema Sendeu.

Alisema TFF isipotimiza makubaliano hayo mpaka kufikia leo saa tano asubuhi, hahawezi kucheza mchezo huo kutokana na kudai shirikisho linatumia mabavu katika kufanya maamuuzi, hivyo na wao sasa wanataka haki yao.

Alisema Berko, juzi alishinda TFF akisubiri kupewa fedha zake,  lakini mpaka siku inamalizika,  hakupewa kitu na hata alipomuulizia Mhasibu, aliambiwa hayupo, wakati alikuwepo ofisini.

Wakati huohuo, Sendeu alizungumzia suala la mshambuliaji wao, Hamis Kiiza 'Diego', ambapo wamempa onyo kutokana na utovu wa nidhamu alioufanya wiki iliyopita wa kuondoka bila kutoa taarifa.

"Kiiza ameomba msamaha kwa uongozi, wachezaji na mashabiki kutokana na kitendo alichofanya, hivyo uongozi umeamua kumpa onyo kwani amekiri kufanya kosa," alisema Sendeu.

Katika hatua nyingine, Sendeu alisema ikiwa mshambuliaji wa Simba kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati, Gervais Kago atacheza katika mchezo huo, ni dhahiri TFF inayumba kwa kukosa msimamo.

Alisema TFF inatakiwa kuwa na msimamo katika maamuzi yake, kwani muda wa kumwombea usajili ulikwisha, sasa wanashangaa kumruhusu kucheza katika mchezo huo.

Alipotafutwa Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura, kuzungumzia hilo, alisema ni kweli wanadaiwa na watawalipa kwani hata serikali inadaiwa, hivyo wanachotakiwa kwa sasa ni kucheza, fedha zao watawalipa.

"Yanga inaleta siasa, kama fedha tayari wamechukua leo asubuhi (jana) za mchezo huo na kama deni mbona hata sisi kuna wakati tuliwakopesha na wakatulipa, sasa iweje wao wanakosa uvumilivu," alihoji Wambura.

Alisema Yanga inavyoonekana wanataka kuharibu biashara ya watu na kwamba, wanaiomba waingize timu uwanjani na mambo mengine ya madeni yatashughulikiwa baadaye.

No comments:

Post a Comment