05 August 2011

Wauza mafuta waitunishia misuli serikali

Na Waandishi Wetu

SERIKALI na waagizaji wakubwa wa mafuta nchini wametunishiana misuli huku kila upande ukishikilia msimamo wake wa kutokubaliana juu ya bei mpya ya bidha hiyo, hali inayodhihirisha kuwa wananchi wataendelea kuathirika zaidi


Mvutano huo ulijidhihirisha Dar es Salaam jana, baada ya serikali kukutana na Chama cha Waagizaji Mafuta nchini (TAOMAC) kwa lengo la kupatia ufumbuzi mvutano baina yao uliosababisha baadhi ya wafanyabiashara hao kufungua vituo wakipinga bei mpya iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati ya Maji na Nishati (EWURA).

Katika mabadiliko hayo, bei hizo ni sh. 2,004 kwa petroli, dizeli sh. 1,911 mafuta taa sh. 1,905.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Engine na Mwenyekiti wa TAOMAC, Bw. Seelon Naidoo ameipa serikali saa 24 kurejesha bei ya awali, vinginevyo hataendelea na biashara hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana akiwa pamoja na wadau hao, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. Eliakim Maswi alisema bei mpya ya mafuta itaendelea kutumika.

"Hapa tumeshakubaliana kuwa bei mpya itaendelea na hivi sasa nakwenda kukagua vituo, na tutakachokuta kimefungwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa," alisema.

Hatua itakayochukuliwa kwa yeyote atakayekaidi agizo hilo, alisema ni kunyang'anywa leseni ya biashara.

Aliongeza kuwa, kwa kuwa tayari wamesikiliza malalamiko ya wafanyabiashara hayo, hivyo serikali itayafanyia kazi na haitakuwa tayari kufanya kazi kwa masharti.

"Serikali haiwezi kupewa masharti ya masaa 24 ila sisi ndio wenye uwezo wa kutoa masharti...kwa kuwa serikali ndiyo inayotoa leseni basi itajua nini cha kufanya," alisema.

Hata hivyo taarifa za ndani zimelieleza gazeti hili kuwa EWURA ilikosea katika kukokotoa hesabu zake ili kufikia bei mpya, hatua ambayo itasababisha hasara kwa wafanyabiashara wa mafuta.

Chanzo chetu ndani ya mkutano huo kilisema jana kuwa katika hesabu hizo, gharama halisi za kampuni za mafuta hazikuzingatiwa, ikiwa tozo ya dola 20,000 kwa siku kila meli ya mafuta inapocheleweshwa ambayo inasababisha gharama ya sh 30 kwa kila lita ya petroli/dezeli.

Jambo jingine ambalo wafanyabiashara hao walieleza ni bei ya manunuzi ya mafuta ambayo huzingatia kanuni ya kimataifa ambayo haikuzingatiwa na EWURA na viwango vya kubadilisha fedha vinavyotumiwa na mamlaka hiyo kudaiwa kuwa chini kwa kati ya sh 2- hadi 30.

Katibu wa TAOMAC, Bw. Salumu Bisarara awali alisema wamekubaliana na uamuzi wa serikali wa kushusha bei ingawa taarifa zimekuwa za ghafla na hawakushirikishwa.

Alisema kuwa kabla ya taarifa hiyo kulikuwa na kikao kilichofanyika Julai 22, mwaka huu lakini cha kushangaza EWURA imetoa bei elekezi kabla ya kujadiliana na wahusika.

"Tumekubaliana na serikali kuendelea na bei mpya wakati ikiendelea kufanya marekebisho kwa mapungufu yaliyojitokeza," alisema.

Hata hivyo, taarifa zililifikia Majira wakati tunakwenda mitamboni zilisema kuwa wafanyabiashara hao waliamua kuendelea na mgomo leo baada ya kupata hasara kubwa kwa muda mfupi ambao baadhi yao walitoa huduma jana.

Vyanzo vyetu vya habari vilisema Kampuni ya Engene ilikuwa imepokea maelekezo kutoka makao makuu yake Afrika Kusini kusimamisha huduma huku BP Tanzania ikisubiri maelekezo baada ya kupata hasara kati ya sh 150 na 170 kwa kila lita ya petroli.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Madini (EWURA), Bw. Haruna Masebu aliwatahadharisha wafanyabiashara hao kutokubali kushawishika na kufunga vituo na kusababisha kero kwa wananchi.

"Kila mtu ana leseni yake, hivyo msikubali kushawishika na kufunga vituo kwa kuwa watashirikiana na vyombo vya dola kukagua na atakayebainika hatua zitachukuliwa," alisema.

Alisema kuwa kabla ya kupunguza kwa bei hiyo waliangalia vipengele mbalimbali ikiwa ni pamoja na faida wanayopata ambapo wafanyabiashara hao wanalalamikia kupata hasara kutokana na mizigo kukaa muda mrefu bandarini na faida wanayopata.

"Tuliweka sh. 7.5 kwa gharama ya usafirishaji, sh. 7.5 kwa gharama za kusafirishia lakini kwanza tuliangalia mtazamo wa kisera na udhibiti, hata hivyo malalamiko yao yatafanyiwa kazi," alisema.

Katika mkutano huo wa dharura wadau 31 walishiriki kutoka kampuni za Total Oil, Oilcom, BP, Petroleum, NSK Oil, Lake Oil, Oryx, Petro Afrika, Engine, Gapco.

1 comment:

  1. Hii ni ya mwananchi newspaper
    Nimeshinda kutuma: Dr. Slaa angeshida...Utafiti.

    Well said, ndugu zangu, mie sijui hali ya nchini mnavyoishi huko ila nasema uchaguzi ukifanyika kwenye magazeti, chama pinzani kitashinda, lakini ukifanyika kwenye vituo kwa kufuata upigaji kura wa kizamani, nasema ushindi utakuwa ndoto!
    Cha kufanya: 1. Jaribuni kupigania utumiaji wa mashine za kura zinazotumia betri (automated election) Philippines waliweza kutumia na matokeo yakajulikana baada ya masaa 24 hadi siku nne.
    2. Mfahamu kuwa wananchi wengi wa tanzania wanaishi vijijini, sijui kwa sasa lakini nilipokuwa hapo miaka mitatu ilyopita CCM ndicho chama kilichojijengea umaarufu vijijini kwa kutumia radio inayowafikia wengi wasio na chumvi (RTD wakati huo).
    3. Kuacha marumbano ya vyama vya siasa ndani kwa ndani kwani watu wakikosa matumaini nyakati za mwisho huamua kuchagua 'zimwi likujualo halikuli ukakwisha'
    4. Utafiti usifanyike si kwa ushabiki wa chama fulani au hasira bali fanyenyeni tafiti za ukati bila kubagua ,wakati na za muda wa kutosha.
    5. Naomba sasa ulizeni je, wanzanzibari wangapi wanaopenda watanganyika na Muungano na nini kifanyike?
    Karibuni watukanaji kunishambulia hata kama hawajasoma kwa makini maoni yangu. Mungu ibariki nchi yetu.

    ReplyDelete