Na Godfrey Ismaely
BAADHI ya wameonesha wasiwasi na kasi ya utendaji kazi ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, huku wakieleza kuwa huenda 'ameminywa', kwa vile
utendaji wake wa sasa si kama alivyoanza awali.
Walitoa hoja hizo wakati wakichangoa mjadala wa bajeti yake ulioitimisha kwa bunge kuipitisha kwa kauli moja.
Mbunge wa Msoma Mjini, Bw. Vicent Nyerere alienda mbali zaidi akitaka Profesa Tibaijuka na naibu wake, Bw. Godluck Ole Medeye wajiuzulu nyadhifa zao kwa vile bajeti yao ya sh. 47 bilioni ni ndogo ikilinganishwa na ukubwa wa mahitaji ya wizara yao.
"Naibu waziri na waziri wake katika hii wizara wanapaswa kutuomba radhi sisi waheshimiwa wabunge na wananchi kwa sababu wametudanganya kwa kuwa fedha walizoomba ni kidogo na hazitoshelezi, kazi ni ngumu katika wizara hii," alisema Bw. Nyerere na kuongeza;
"Kwa vile wametudanganya wajiuzulu mara moja na kama walishindwa kuomba fedha za kutosha na hata kumueleza rais juu ya umuhimu wa mahitaji ya wizara yao waniambie mimi nikikutana na yeye nitamueleza hayo yote," aliongeza.
Alisema kama wizara hiyo itashindwa kuomba radhi juu ya fedha ilizoomba na hata kufikia hatua ya kujiuzulu basi itafika hatua utekelezaji wa majukumu yao ukafikia mahali ukakwama kutokana na migogoro mbalimbali ya ardhi pamoja na uhitaji mkubwa wa maofisa wa kupima ardhi ili kutoa fursa sawa kwa wananchi.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Bi. Suzan Kiwanga, alitilia shaka utendaji kazi wa wizara hiyo na kuhoji iweje katika miaka 50 ya uhuru asilimia moja tu ya ardhi ndiyo imepimwa.
"Mnafanya nini! Eti kupima ardhi asilimia 100, eti itachukua miaka laki moja? Haiwezekani kama mmeshindwa kaeni pembeni, wengine wenye uwezo waingie waendelee kuhudumia ardhi," alisema Bi. Kiwanga na kuongeza;
"Serikali ipo kama haipo. Hao maofisa ardhi wanafanya nini hadi wizara mnashindwa kuwasimamia? Kwa hili lazima lifanyiwe kazi haraka." Alitoa mifano mbalimbali ya migogoro ya ardhi hasa katika wilaya ya Kilombero huku akimtuhumu mbunge mmoja kuwa amewarubuni wananchi kwa sh. 1,000 kila mmoja ili waidhinishe kumpatia zaidi ya hekari 300 za ardhi.
"Mbunge wa Kisesa anapaswa kurudi huko Shinyanga, siyo kwenda Kilombero na kutoa sh. 1,000 na mipira ili wananchi waidhinishe hoja zake...hiyo ni rushwa, abaki huko huko Kisesa, kwani yeye amekuwa wa viti maalum? "alihoji.
Wakati huo huo, Naibu Spika, Bw. Job Ndugai maeungana na wabunge kuwatuhumu watendaji na wenyeviti wa vijiji kuwa wanagawa ardhi wanavyotaka kwa madai wanatumia vibaya sheria ya ardhi ya vijiji.
Bw. Ngudai alitoa shutuma hizo jana bungeni mjini Dodoma wakati akifunga kipindi cha majadiliano katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
"Watendaji wanatumia vibaya sheria ya ardhi ya vijiji kwa kugawa vibaya ardhi ya wanakijiji hivyo kuchangia migogoro ya mara kwa mara mfano kule kwangu Kongwa na hata tukiangalia katika maeneo ya Kilombero na Babati," alisema Bw. Ndugai.
Shutuma za Naibu Spika zilienda sambamba na zile za Mbunge wa Karatu Mchungaji Israel Natse ambaye wakati akichangia katika hoja hiyo alisema kuwa baadhi ya watendaji wa serikali wanahusika kugawa ardhi bila kuwashirikisha wananchi moja kwa moja hivyo kuchochea migogoro ya mara kwa mara.
"Kuna tabia za watendaji kunyakua ardhi za wananchi na kuigawa kwa wawekezaji bila kuwashirikisha wahusika, hali hiyo ndiyo chanzo cha migogoro ya ardhi kwa kuwa wanaingia mikataba na wawekezaji bila ushirikiano," alisema Mchungaji Natse.
Kwa upande wake Mbunge wa Lushoto, Bw. Henry Shekifu (CCM) alisema iwapo serikali itashindwa kuwasimiamia watendaji pamoja na maofisa ardhi vyema wataipeleka nchi pabaya kwa kuwa ndio chanzo cha migogoro ya ardhi.
"Maofisa wa Ardhi na wakuu wa wilaya wanapaswa kutenda haki kwa wananchi kwa kuzingatia misingi ya katiba, kwani wao ndiyo chanzo cha migogoro hivyo kusababisha wananchi kukosa matumaini na serikali yao," alisema Bw. Shekifu.
Serikali dhalimu imeshamminya huyu mama, Hata aje malaika, hataweza kubalidilisha Tanzania chini ya CCM.
ReplyDeleteUfisadi na uroho wa pesa ndo wanajua tu viongozi wa CCM. Hata wabunge wanapelekewa Bahasha za Rushwa!!!
Dawa ni kuindoa CCM tu, iwe ni kwa kura au maandamano.
Wananchi wa Tanzania waelimishwe waache uoga maana haki haiombwi, hudaiwa kwa nguvu.
Maaandamano makubwa yaja, mafisadi kaeni chonjo