11 August 2011

Twiga Stars yatolewa nje za kirafiki

TIMU za soka za wanawake za Afrika kusini na Zimbabwe, zimekataa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa  ya Twiga Stars.


Twiga Stars inajiandaa na fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika nchini Msumbiji mwezi ujao.

Timu hizo zimekataa mechi hiyo ya kujipima nguvu kabla ya kwenda Msumbiji kwa madai kuwa, zimepangwa kundi moja.

Twiga Stars imepangwa Kundi B, ikiwa na timu za Afrika Kusini, Msumbiji, Zimbabwe na Ghana, ambapo Septemba 5, itaumana na timu ya taifa ya Ghana 'Black Princesses'.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF, Bonifance Wambura, alisema timu hizo zimetoa sababu nyingi na za msingi, hasa ya kuwa kundi moja kwenye michuano ambayo zinatarajiwa kukutana.

"Ukiangalia ni siku chache zimebaki, sababu walizotoa ni za msingi, hivyo tumeachana nazo na kugeukiwa upande mwingine," alisema Wambura.

Alisema baada ya nchi hizo kukataa kucheza mechi ya kirafiki, wanafanya mawasiliano na timu za Botswana, Zambia na Malawi ili kikosi hicho kiweze kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa kabla ya kwenda mjini Maputo.

Naye Kocha Mkuu wa Twiga Star,  Charles Mkwasa, alisema mchezo wa kujipima nguvu utasaidia kujua viwango vya wachezaji wake.

Kikosi chake kinaendelea na mazoezi kikiwa na wachezaji 25, na kuweka kambi Msimbazi Center, Dar es Salaam.

Kambi ya kikosi hicho inasimamiwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), ambao wanawahudumia wachezaji 20, lakini TFF imewaongeza wanne na kuwagharamia.




No comments:

Post a Comment