29 August 2011

'Tatizo la nchini umeme kukwamisha mradi wa ET,

Na Tumaini Makene

WAKATI baadhi ya walimu wakionesha matumaini juu ya ufanisi katika ufundishaji na kujifunza unaopatikana kutokana na Mradi wa Elimu Teknolojia (ET), bado wameonesha
mashaka iwapo teknolojia hiyo itaweza kutumika ipasavyo na kuwa sehemu ya mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu nchini, kwani tatizo la nishati ya umeme litaathiri mradi huo kwa kiasi kikubwa.

Mradi wa ET unaoendeshwa na shirika lisilokuwa la serikali la International Youth Foundation (IYF) kwa udhamini wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID), unahusisha matumizi ya simu na video katika ufundishaji wa masomo ya sayansi kwa shule za msingi, ambapo unawawezesha wanafunzi kujifunza mitaala ya masomo hayo kwa kuona.

Wakizungumza mwishoni mwa wiki mjini Dar es Salaam, wakati wa warsha ya kuwapatia mafunzo ya mradi huo wa ET, kwa mara nyingine kabla ya haujakabidhiwa rasmi kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (WEMU) ili uendeshwe na serikali, baadhi ya walimu walisema pamoja na umuhimu wake, bado suala la umeme litakuwa kikwazo kikubwa.

Ofisa Taaluma wa Wilaya ya Ilala, Bi. Hilda Shallanda, alisema katika maeneo ya majaribio ya mradi wa ET, umeonesha kurahisisha ufundishaji, hivyo alitoa mwito kwa kila mdau wa elimu nchini, kuhakikisha anatimiza wajibu wake.

"Zipo changamoto kadhaa, mojawapo ikiwa ni suala la umeme maana hata kama tutaamua kutumia sola au jenereta maana yake tutahitajika fedha za kununulia , kingine ni iwapo waliopata elimu hii hawataitumia vizuri, ni muhimu sasa twende na wakati, wale ambao wameipata waende wakafundishe wengine," alisema Bi. Shallanda.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Manzese, Bw. Joe Kihampa aliitaka serikali kuwa makini kuendeleza miradi inayokabidhiwa na wafadhili ili ufanisi ulioonekana wakati wa majaribio ya ET, uendelee vivyo hivyo.

Alishauri bei za simu na luninga zipunguzwe hasa kwa kuzingatia kuwa ndizo zinazotumika kutoa elimu hiyo.

Bw. Kihampa alisema IYF imefanya kazi kubwa katika kuufanikisha mradi huo, hivyo wahusika wengine wahakikishe unaendelea.

Naye Mtaalam wa Elimu na Utoaji Mafunzo wa IYF, Bi Zamaradi Saidi, alisema hadi sasa shirika hilo limeshachukua hatua kadhaa kuhakikisha vifaa vinavyotumika katika utoaji wa elimu hiyo, hasa simu na Tv, vinapatikana kwa gharama  nafuu.

Majaribio ya ET yalianza mwaka 2008, ambapo WEMU imekuwa ni mshirika mkuu, ukilenga kutumia teknolojia katika kuboresha ufundishaji na elimu kwa ujumla, hususan kwa shule za msingi, ambapo hadi sasa shule 150 katika wilaya 17 nchini zimenufaika.


No comments:

Post a Comment