Na Mwali Ibrahim
CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimeteua Kamati ya Tamasha la Michezo la Miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika linalotarajia kufanyika
Novemba 5, mwaka huu Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto alisema kamati hiyo itakuwa na waandishi 16 kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Alisema kamati hiyo itaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Uhariri ya gazeti la Raia Mwema, Johnson Mbwambo, Mhariri Mkuu wa gazeti la Spoti Starehe, Masoud Sanani ambaye atakuwa Makamu Mwenyekiti na wajumbe ni Said Salim ambaye ni mhariri mkongwe na Mwalimu wa waandishi wa habari.
Wengine ni Mhariri wa gazeti la This Day, Willy Chiwango, Asha Muhaji Mhariri Leap Media, Rashid Zahoro Mhariri gazeti la Burudani na George John Katibu Msaidizi TASWA.
Mahmoud Zubeiry Mhariri Dimba, Mohammed Mkangara Mhazini Msaidizi TASWA, Juliana Yassoda Naibu Mkurugenzi Idara ya Michezo, Majuto Omary Mwenyekiti TASWA FC na Ephraim Kibonde Mtangazaji Clouds FM.
Wajumbe wengine ni Deo Rweyunga Mkurugenzi Radio One, Chacha Maginga Mtangazaji TBC1, Amour Hassan Mhariri Nipashe na Zena Chande TASWA.
Katika hatua nyingine TASWA, imeiagiza Sekretarieti yake kuzungumza na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kuhusu kutenga eneo watakalokaa waandishi wakiwa katika Uwanja wa Taifa katika kuripoti mechi mbalimbali.
Hatua hiyo ya TASWA, imetokana na hivi karibuni waandishi mbalimbali wa michezo kutolewa maneno machafu na mashabiki wa soka na wengine kupigwa wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao uwanjani, kutokana na kukaa pamoja na mashabiki hao.
Pinto alisema, TASWA inaitaka TFF iwaoneshe eneo lililotengwa miaka ya nyuma kabla uwanja haujaanza kutumika ambalo ni maalumu kwa ajili ya kukaa waandishi wa habari za michezo, ili isaidie kupunguza matatizo hayo.
Kutokana na hali hiyo TASWA, inalaani kitendo cha mashabiki wa mpira wa miguu ambao si wastaarabu na imewataka kuthamini mchango wao kwa faida ya mashabiki waliopo mbali na uwanja.
No comments:
Post a Comment