Na Zahoro Mlanzi
TIMU ya Azam FC, imechagua Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kwa ajili ya mechi zake za Simba na Yanga za Ligi Kuu Bara.Timu hiyo awali ilitoa taarifa kwa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), baada ya Uwanja wa Uhuru kufungwa kupisha matengenezo kwamba itazifuata timu hizo katika viwanja vitakavyochagua.
Yanga na Simba ilichagua kutumia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa mechi za ligi lakini baadaye serikali ikaufunga uwanja huo kwa ajili ya matengezo, hivyo timu zitalazimika kutafuta viwanja vingine.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Jaffar Idd alisema uongozi wa timu hiyo umeamua mechi hizo zikachezwe Mwanza ndipo walipoona kunaifaa timu yao kwani nyasi zake zipo katika kiwango kizuri.
Alisema walitarajia jana kuwasilisha barua TFF kuwataarifu kwamba watatumia uwanja huo kwa mechi za Simba na Yanga, ambazo timu hiyo itakuwa mwenyeji.
"Baada ya uongozi kuliona hilo muda wowote barua itapelekwa TFF, kama unavyojua uwanja wetu kule Chamazi hautaweza kuchukua mashabiki watakaoingia katika mechi hizo, hivyo tumeona uwanja huo utatusaidia," alisema Idd.
Alipoulizwa Ofisa Habari wa TFF kwa simu, Boniface Wambura kuhusu suala hilo na kama barua imewafikia, alisema kama Azam wamechagua uwanja huo itabidi wakae waliangalie upya kwani walishatangaza watazifuata timu hizo zitakapokuwa.
"Kama wanasema hivyo ni dhahiri si jambo la juu juu, kama mnavyojua tulitoa muda kwa timu zinazotumia uwanja wa Uhuru zichague viwanja vingine kupisha matengenezo na wao (Azam) wakasema wanatumia uwanja wao, lakini kwa Simba na Yanga watachezea uwanja watakaotumia na wakati ule ulikuwa ni Taifa," alisema Wambura.
Alisema kwa sasa anachofahamu Yanga ipo Morogoro na Simba imechagua Tanga, hivyo suala hilo litabaki kama lilivyo kwa Azam kuzifuata timu hizo zilipo mpaka uamuzi mwingine utakapotolewa.
No comments:
Post a Comment