Na Amina Athumani
TIMU ya Taifa ya netiboli 'Taifa Queens', imeifunga timu ya Filbert Bayi iliyojaa wachezaji wa kimataifa magoli 36-31, katika mechi ya kirafiki kujiandaa na michuano ya
Afrika (All Africa Games; itakayoanza Septemba 3, mwaka huu.
Taifa Queens ni moja ya timu zitakazowakilisha nchi kwenye mashindano ya All Africa Gmes yatakayofanyika mjini Maputo, Msumbiji.
Filbert Bayi, iliongozwa na wachezaji watatu wa kimataifa kutoka Malawi, Takondwa Lwazi, Beauty Chirwa na Mary Angelo.
Katika mechi hiyo, Filbert Bayi aliipeleka pita timu ya Taifa, ingawa walizidiwa mabao machache katika mchezo huo.
Katika kipindi cha kwanza, Taifa Queens walimtumia vizuri Mwanaidi Hassan, na kuongoza kwa mabao 12-7.
Kipindi cha lala salama, kila timu iliingia ikiwa na nguvu mpya baada ya kupata maelekezo kutoka kwa makocha wao.
Filbert Bayi ilikuwa ikiongozwa na Kocha Mary Angel, wakati Taifa Queens wakiwa chini ya Mary Protus 'Super Coach'.
Taifa Queens mpaka dakika za mwisho, iliibuka na ushindi wa mabao 36-31.
Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika, kocha wa Taifa Queens, Mary, alisema mchezo huo umewapa changamoto kubwa kwani amegundua mapungufu yaliyopo katika kikosi chake.
Mary alisema kuwa, mapungufu hayo atafanyia marekebisho kabla ya kuelekea mjini Maputo.
Kocha huyo alisema, kikosi chake kinatakiwa kipate mechi nyingine za kirafiki ili kijiweke katika nafasi nzuri ya kushinda mjini Maputo.
Alisema wanategemea kujitupa tena uwanjani kumenyana na timu ya Kombaini ya Mkoa wa Dar es Salaam, wakati viongozi wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) na CHANEZA, vikiendelea na utaratibu wa kutafuta mechi nyingine.
No comments:
Post a Comment