BOGOTA, Colombia
TIMU ya Taifa ya vijana ya Brazil, imetwaa ubingwa wa fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wenye miaka chini ya 20, baada ya kuifunga Ureno mabao 3-2, katika
mchezo wa fainali uliofanyika mjini Bogota, Colombia, juzi.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Marekani (AP), mabao matatu yaliyofungwa na Oscar, ndiyo yaliifanya timu hiyo kuibuka na ushindi huo katika muda wa dakika za nyongeza.
Oscar aliipatia bao la ushindi timu yake dakika ya 111 kwa shuti kali lililogonga mwamba wa juu, kabla ya kutumbukia kimiani.
Kabla ya bao hilo kufungwa, mchezaji huyo alikuwa ameifungia timu yake mabao mawili, dakika ya tano na 78.
Mchezaji Alex ndiye aliyeanza kuzitikisa nyavu za Brazil dakika ya tisa na Nelson Oliveira akaongeza lingine dakika ya 59 na kuifanya timu hiyo iwe mbele kwa muda.
Hata hivyo, baada ya kupachikwa mabao hayo, Brazil ilipigana kufa na kupona, ikatoka nyuma na kufanikiwa kutwaa ubingwa huo kwa mara ya tano, ikiwa ni baada ya kushika nafasi hiyo miaka miwili iliyopita.
"Ushindi huu umetufanya tujisikie wenye furaha, kwa sababu tumefikisha rekodi ya timu ya wakubwa," Kocha wa Brazil, Ney Franco, alisema wakati akifananisha ubingwa huo na ubingwa wa timu ya wakubwa.
Kwa upande wake Kocha wa Ureno, Ilidio Vale, alisema matokeo hayo yalikuwa ni ya haki, huku akikubali kuwa, kiwango cha Brazil kilikuwa cha juu sana.
No comments:
Post a Comment