19 August 2011

Muro: Waziri Masha alinitisha

Na Rehema Mohamed

MSHTAKIWA wa kwanza katika kesi ya kuomba rushwa ya sh. milioni 10 inayomkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Bw. Jerry Muro na
wenzake wawili ameiambia mahakama kuwa aliwahi kutolewa maneno ya vitisho na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Bw. Lawarence Masha.

Bw. Muro alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu, Bw. Frenk Mushi wakati akitoa utetezi wake akiongozwa na wakili wake Bw. Richard Rweyongeza.

Bw. Muro alidai mahakamani hapo kuwa Bw. Masha alitoa kauli hiyo katika Ofisi za TBC wakati alipokwenda kwa ajili ya kuonana naye.

Bw. Muro alidai kuwa Bw. Masha alifika ofisini hapo saa mbili usiku akiwa ameshika bahasha ya kaki ambapo baada ya kumuona Bw. Muro alimuambia amekwisha na kutupa chini.

"Baada ya kusema hayo akasema mimi nitaondoka na wewe lazima uondoke, si unaona wananchi wanavyolalamika kuhusu Jeshi la Polisi, akaniambia tazama hizo picha, nilimuuliza za nini?, akasema si unajiona ukiwa na mataperi wakubwa hapa mjini.

"Niliokota ule mfuko ambapo ndani kulikuwa na picha tatu alizodai za CCTV ambazo zilionesha watu watatu ambao sura zao hazikuonekana vizuri ambazo alidai mimi ni mmoja wapo," aliongeza.

Bw. Muro alidai kuwa baada ya hapo mfanyakazi mwenzake, Bi. Jane Shirima alimuuliza kitu cha kufanya ambapo Bw. Masha alimtaka aitishe mkutano na waandishi wa habari aseme kuwa Jeshi la Polisi halikumuonea kumkamata ila waligongana.

Alidai kuwa baada ya hapo alimueleza hali hiyo aliyekuwa bosi wake kwa wakati huo, Bw. Tido Mhando na kumshauri kuwa asiitishe mkutano huo kwani mwenye jukumu hilo ni Bw. Masha na wao watapeleka waandishi kuchukua habari.

Alidai kuwa baada ya kupewa ushauri huo alimpigia simu Bw. Masha kumueleza hayo ambapo alimjibu kuwa alishamalizana naye na anakwenda Dodoma kumueleza Waziri Mkuu.

Aidai kuwa tuhuma anazokabiliwa nazo zimemfanya ajione kama yupo kaburini kwani amesimamishwa kazi na sasa hapewi malipo yoyote kutoka kazini kwake.

Aliongeza kuwa hali hiyo imemfanya afukuzwe katika nyumba aliyokuwa amepanga Mbezi Beach, kukataliwa kusoma katika Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, pamoja na kunyimwa fedha dola 4,000 za tuzo ya mwandishi bora Tanzania kutoka MCT.

"Wakati nikiwa naendelea na kesi nilipata barua kutoka MCT ikinikumbusha tuzo niliyopata na kueleza sitapewa fedha hizo hadi kesi itakapokwisha huku barua ikionesha mwisho wa kuzichuwa kuwa Desemba 30, mwaka jana," alidai Bw.Muro.

Washtakiwa wengine ni Bw. Edmund Kapama pamoja na Bw. Deogratius Mgasa na kesi hiyo imehairishwa hadi Septemba 27, mwaka huu

3 comments:

  1. kazi ni kwako Murro , tamaa mbele mauti nyuma sasa majuto . masha hahusiki na hayo hakukwambia ukachukue rushwa .

    ReplyDelete
  2. Wewe mtoa maoni- una lako jambo una uhakika ya kwamba Muro alichukua rushwa? Wacha kesi iendelee mpaka mwisho ili tujue ukweli wake.

    ReplyDelete
  3. Huyo mtoa maoni anaongea kama anakwenda namaji, cha muhimu tuwaombee kwa mungu wawe na afya njema bro muro na masha ili haki tuiyone wakiwa hapahapa dunian.

    ReplyDelete