29 August 2011

Majambazi yavamia wachimbaji, yauawa

Na Livinus Feruzi, Bukoba

MAJAMBAZI watatu wameuawa na wananchi baada kuvamia mgodi wa dhahabu wa Matabe uliopo eneo la Nyampalahara Wilaya ya Chato, Mkoa wa
Kagera .

Katika tukio hilo majambazi wengine watatu akiwemo mwanamke mmoja, walifanikiwa kutoroka na kuelekea kusiko kusikojulikana .

Kamanda wa Polisi wa Polisi Mkoa wa Kagera, Bw. Henry Salewi, aliwaambia waandishi wa habari kuwa watu sita wanaodhaniwa majambazi  wakiwa na bunduki moja aina ya AK47 yenye namba UC-1649-1998 na mapanga, walivamia mgodi huo Agosti 25 kwa lengo la kufanya uporaji kwa wachimbaji wa dhahabu.

Kamanda Salewi alisema baada ya kuwasili mgodini hapo, wachimbaji walipeana taarifa na kuanza kupambana nao, ambapo wachimbaji watano walijerujiwa katika tukio hilo, akiwemo aliyepigwa risasi tumboni.

Alisema majambazi hao  watatu waliouawa hadi sasa bado hawajatambuliwa, na kuwa bunduki ambayo polisi wamefanikiwa kuikamata inadhaniwa kuwa ya Burundi kutokana na nembo yake inavyoonesha.

Bw. Salewi alisema wachimbaji watano waliojerujiwa katika tukio hilo, wawili wametibiwa na kuruhusiwa, lakini wengine watatu ambao majina hayajapatikana kutokana na kuwa na hali mbaya wamelazwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Chato kwa matibabu.

Alisema  maganda mawili ya risasi aina ya SMG na risasi tatu ambazo zilidondoka wakati wa purukushani zimeokotwa.

Alisema miili ya watu hao imehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Chato. Alisema Jeshi la Polisi linaendelea na kuwasaka majambazi watatu walitoroka na kuwaomba wananchi kutoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwao,  huku  taarifa za siri zilizopatikana zimedai kuwa watu hao walitokea eneo la Runzewe.

No comments:

Post a Comment