24 August 2011

Jairo hana hatia-CAG

*Luhanjo aamuru aanze kazi leo
*Asema hakupatina na kosa lolote


Na Grace Michael

KATIBU Mkuu Kiongozi Bw. Phillemon Luhanjo ameamuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Bw. David Jairo kurejea
mara moja kazini kwa kuwa uchunguzi uliofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) haujamkuta na hatia yoyote.

Bw. Jairo, ambaye alisimamishwa kazi Julai 21, mwaka huu ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zilizotolewa bungeni wakati wa kuwasilisha wa hotuba ya bajeti ya Wizara yake ambapo alidaiwa kuchangisha jumla ya sh. bilioni moja  kuwahonga wabunge wapitishe bajeti ya wizara hiyo.

Akitoa uamuzi juu ya uchunguzi uliofanywa na CAG dhidi ya tuhuma hizo, Bw. Luhanjo alisema: “Kutokana na matokeo haya ya uchunguzi wa awali ambao umefanywa kwa umakini mkubwa na kushindwa kuthibitisha tuhuma hizo, mimi kama Mamlaka ya nidhamu ya Katibu Mkuu wa Nishati na Madini David Jairo, sitaweza kuendelea na hatua ya pili ya kumpa taarifa ya tuhuma na hati ya mashtaka kwa kuwa Jairo hajapatikana na kosa lolote la kinidhamu,” alisema Bw. Luhanjo.

Kutokana na hatua hiyo, alisema kwa mujibu wa sheria namba 8 ya Utumishi wa Umma
na kanuni zake anamwamuru Bw. Jairo kurejea kazini mara moja ambapo atatakiwa
kuingia ofisini kwake leo.

Akifafanua matokeo ya uchunguzi wa tuhuma hizo, CAG Ludovick Otouh alianza kwa kueleza chimbuko la uchunguzi huo ambapo alisema ulitokana na wabunge waliohoji uhalali wa wizara kuomba michango kutoka kwenye taasisi kwa lengo la kushawishi baadhi ya wabunge kupitisha bajeti kirahisi.

Alisema kuwa ukaguzi huo ulifanyika kulingana na hadidu rejea zilizokuwa na lengo la kutafuta ukweli kuhusu tuhuma za michango na matumizi ya fedha zilizochangwa na wizara.

“Kazi hii ilihusisha kufanya mapitio ya nyaraka mbalimbali, vitabu vya risiti, hati
za malipo na taarifa za benki kwa kipindi cha mwezi Mei hadi Julai mwaka huu na timu
ya wakaguzi iliwahoji watu kutoka taasisi zilizochangishwa, wizara, wabunge na
wakala wa Jeolojia Tanzania," alisema CAG.

Alisema ukaguzi ulibaini kuwa idadi ya taasisi zilizopewa barua za kuchangia gharama
za kuwasilisha bungeni bajeti ya wizara zilikuwa ni nne na sio 20 kama ilivyokuwa
ikidaiwa na wabunge na utafiti huo ulibaini kuwa jumla ya fedha zilizochangwa ni sh.
milioni 149.7.

Mbali na fedha hizo zilizochangwa na taasisi lakini pia ukaguzi huo ulibaini kuwa idara ya uhasibu ya wizara ilitoa sh. milioni 150.7 kwa ajili ya posho za vikao vya kazi katika uandaaji wa uwasilishwaji wa bajeti hiyo lakini pia Idara ya Mipango ya wizara nayo ilichanga sh. milioni 278 kwa ajili ya kazi hiyo.

Aidha CAG alifafanua kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) iligharamia
chakula cha mchana cha sh. milioni 3.6 na tafrija iliyofanyika Julai 18, mwaka huu
ambayo iligharimu sh. milioni 6.1.

“Jumla ya michango iliyochangwa ni sh. milioni 578.5 na sio bilioni moja kama ilivyotajwa kwenye tuhuma na taasisi zilizodaiwa kuhusika sio 20 kwa kuwa wizara hiyo ina taasisi zisizo zidi saba,” alisema Bw. Otouh.

Ukaguzi huo pia haukupata ushahidi wowote wa fedha zilizochangwa kutumika kuwalipa
wabunge malipo yoyote kwa madhumuni ya kuwahonga bali malipo yaliyofanyika yalihusu
posho za kujikimu, takrima na posho za vikao kwa maofisa walioshiriki katika kazi
nzima ya uwasilishwaji wa bajeti.

Kwa mujibu wa taarifa za benki iliyotumika kukusanya fedha hizo hadi kufikia Julai
29, mwaka huu kiasi cha sh. milioni 20 kilikuwa ni fedha za matumizi ya fedha zilizochangwa na kupokelewa kwenye akaunti ya GST kabla ya kufanyika marejesho ya sh. milioni 99.4 na sh. milioni 14.8.

Kutokana na hali hiyo, CAG alisema kuwa jumla ya kiasi cha fedha kilichosalia kwenye
akaunti hiyo kulingana na nyaraka za benki ni sh. milioni 195.2.

“Kwa kuwa ukaguzi maalum haukupata uthibitisho wa kuwepo taasisi 20 zilizotakiwa
kuchanga bilioni moja kama ilivyodaiwa na wabunge, ukaguzi haukuthibitisha kuwepo
kwa usahihi wa tuhuma zilizotolewa dhidi ya Bw. Jairo,” alihitimisha CAG.

Hata Hivyo waandishi wa habari walipohoji ni kwa nini vyombo vingine vya dola ikiwamo
TAKUKURU na polisi havikuhusishwa kwenye uchunguzi huo, Bw. Luhanjo alisema kuwa suala
hilo lilikuwa ni tatizo la kiutawala wa kifedha na sio rushwa wala kosa la jinai.

Alitumia mwanya huo, kuwaonya watumishi wa umma wanaojihusisha na uvujishaji wa siri na nyaraka za serikali kwa kuwa kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa umma.

“Hata huyu aliyefanya hivi tukimpata naye atapata haki yake...ni kosa kubwa kuvujisha siri za serikali kwani usalama wa serikali ni wa mtumishi mwenyewe hivyo natoa onyo na iwe fundisho kwa watumishi wengine wenye tabia za kutoa siri za serikali,” alisema Bw. Luhanjo.

Hatua ya kusimamishwa kwa Bw. Jairo ili kupisha uchunguzi ilitokana na tuhuma zilizotolewa na wabunge wakati wa bajeti ya awali ya Wizara ya Nishati na Madini ambapo walidai kuwa Bw. Jairo amechangisha jumla ya sh. bilioni moja kutoka kwenye taasisi 20 zilizo chini ya wizara hiyo kwa lengo la kuwahonga wabunge kupitisha
bajeti hiyo.



11 comments:

  1. JK UNAIPELEKA PABAYA TANZANIA.

    ReplyDelete
  2. Utawala wa sheria huo. Ama kweli rushwa hadi ikulu!

    ReplyDelete
  3. kwani JK ndiye aliyefanya uchunguzi,kuwen wawaz km aliyefanya uchunguz ni CAG semen awe makin,Jk hawez kusimamia shughuli zote,na ndio maana kuna Idara mbalimbali,mchukieni mtu ila msipitilize,Yangu ni hayo.

    ReplyDelete
  4. Namwombea JK kwa Mwenyezi Mungu ili amalize kipindi chake kwa amani. Mimi huwa nashangaa sana maana kila jambo likitokea baya wa kulaumiwa ni Jakaya Kikwete,JK,JK! Je hatuoni wengine? Naungana na mwenzangu aliyetoa maoni yake hapo juu. Kama kuna mtu ana chuki na JK basi ana lake jambo. JK ni binadamu kama wewe na mimi na wala si malaika na kama sisi Watanzania itakuwa ni kuona yale mabaya tu ya mtu bila kuona kuyaona mema yake na kumsaidia kutuongoza basi hata yule ajaye itakuwa hivyo hivyo.

    ReplyDelete
  5. Watanzania wengi ni mataahira kila kinachosemwa na wanasiasa wao wanaamini kutokana na ushabiki wa vyama vyao. mdomo mwingi tu na uzushi,sasa si mnao mawakili waliosheheni huko upinzani nendeni mahakamani. Lymo wa chadema kashutumiwa kuhusika na mtandao wa majambazi na katibu wake juzi kakamatwa,sasa tumfunge Lymo? si kasemwa kuwa jambazi na katibu wake kakamatwa jambo linaloashiria wazi kuna jambo katika ofisi ya Lymo. acheni pumba

    ReplyDelete
  6. Kiongozi wa DP alisema Vasco Da gama ni g..d

    Kama Vasco ni legelege why walio chini yake wasimchezee?

    ReplyDelete
  7. JK kama kiongozi anatakiwa achukulie hatu mambo mengine na sio kukodoa macho tu na kucheka.Kwa stahili hii tuliyokuwa nayo hata chenge na wanzake tutaambiwa hawana hatia.Nyie watu wengine mashabiki maandazi wacheni kutetea kila jambo.Baba wa nyumba akiwa legelege hataweza kuweka nithamu nzuri katika familia yake.Hapa tukubali tu ufuatiliaji wa kila uwozo unaofanya ni mbovu.

    ReplyDelete
  8. Hakuna mtu mwenye jambo na JK kama raia. Tatizo linakuja pale anapokaa kimya wakati watu aliowateua yeye (na ni yeye tu anayeweza kuwatoa) wanapoangamiza taifa na yeye yupo halafu anawatazama tu. Ni wazi kuwa ninyi mnaomtetea hamjui mamlaka na majukumu aliyonayo. Yeye ni binadamu, sawa kabisa, lakini je, ina maana kwa kuwa yeye ni binadamu basi hawezi kufanya chochote? Mnataka watu wafanye nini wapoona taifa linaangamia wakati rais yupo? Unathubutu kumwombea amalize kipindi chake salama, ni usalama gani ambao wewe/ninyi mnauona? Hivi watu mmekuwa na roho ngumu kiasi cha kujivika mabomu na kuombea kipindi kipite salama? au ndiyo mmejizira?
    mtu akifanya mema, hatuna haja ya kuyazungumzia, kwa kuwa ndiyo tunayotegemea ayafanye. akifanya mabaya au akiyanyamazia yanapofanyika hasa yapohatarisha usalama wa taifa zima, hatuwezi kunyamaza na kusubiri kuangamia. Tutazungumza, tutapiga kelele, tutaandamana au vinginevyo ili mradi hata kama tutakufa, basi tufe baada ya kuwa tumejishughulisha.

    ReplyDelete
  9. Wewe Anonymous unayezungumzia kwamba watanzania tunafata ushabiki na siyo ukweli unajisema mwenyewe. Kwanza taarifa yako uliyoandika hapa si sahisi. Aliyepakaziwa tuhuma hizo unazotaka tuziamini ni Mbunhe aitwaye Lema na si Lymo. Pia huyo siyo katibu wake, ila alishawahi kuwa katibu wake. Nawewe unauhakika gani na habaari hizi zilizotolewa na magazeti chochezi ya serikali yanayotaka kuuwa upinzani wa kweli. Watu kama nyinyi ndiyo mnaoturudisha nyuma. Mnafikra mgando na hamtaki kujielimisha hata kwa mambo madogo muhimu. Uwe mfatiliaji mzuri wa mambo, na si kupayuka kuonyesha ujinga wako kwenye uwanja kama huu.

    ReplyDelete
  10. Ndiyo maana tunalilia katiba mpya, hii iliyopo imempa madaraka makubwa raisi, sasa kutokana na nchi kukua na changamoto kuongezeka ndiyo maana anashindwa kufatilia mambo kiufasaha. Yeye ndiye anawateuwa Makatibu, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi mbalimbali nk. Ukishateuliwa na Rais, mtu baki hawezi kukuingilia maana unawajibika kwa Rais. Ndiyo maana kwenye hili, lawama zinabakiwa kwa Mh. Rais kutokana na ukimya wake.

    ReplyDelete
  11. Ama kweli Ikulu imeingiliwa. Yaani utetezi wa Bwana Luhanjo hauingii akilini hata kidogo. kinachoonekana ni utamaduni ule ule wa kulinda mkubwa mwenye "ulaji" na mfujaji na kumtafuta mlalahoi aliyefichua uozo ili ikiwezekana aning'inizwe. Mpaka hapo bado tuna Ikulu kweli? Yaani tumefika mahali ambapo, taarifa za WIZI na ufujaji wa fedha za Umma tunazipa hadhi ya kuziita siri za serikali! Sijui hawa wanaojiita viongozi wetu walisoma shule zipi ambako watu hufundishwa jinsi ya kuliibia taifa bila HURUMA wala HAYA na bado ukaendelea kujoota kiongozi.

    ReplyDelete