Na Severin Blasio, Morogoro
TIMU ya soka ya Assembly ya mjini Morogoro, imewataka wachezaji wake waripoti kambini haraka kwa ajili ya kujiandaa na Ligi ya Taifa Manispaa ya Morogoro msimu ujao.
Akizungumza mjini Morogoro jana, Katibu Mkuu wa timu hiyo, Daudi Julian, alisema mazoezi hayo yatakuwa yakifanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Msamvu kuanzia wiki ijayo, chini ya Kocha Charles Sendwa 'Timbe'.
Alisema Assembly imeamua kuanza mazoezi mapema wakiwa na lengo la kuhakikisha, wanakuwa na kikosi imara chenye ushindani katika ligi hiyo.
"Maandalizi ya mazoezi yanakwenda vizuri, uongozi umejipanga vizuri kuhakikisha timu inafika mbali mwaka huu," alisema.
Alisema timu hiyo itaundwa na wachezaji wenye umri chini ya miaka 20, lengo lao likiwa ni kutoa nafasi zaidi kwa vijana kucheza mpira kama ilivyo katika nchi nyingi zilizoendelea kisoka.
Alisema mbali na mazoezi hayo, timu hiyo baada ya kujifua itacheza mechi nyingi za kirafiki ndani na nje ya Morogoro.
Alizitaja baadhi ya itimu walizopanga kukutana nazo ni Kihonda Magorofani, Jamaica, Moro Kids, Chipolopolo, Kaizer Chiefs, Mikese Academy, Soweto Rangers na Black Viba.
Julian ametoa wito kwa wanasoka chipukizi wa Morogoro, kujitokeza kwenye mazoezi ili waweze kusajiliwa na timu hiyo.
No comments:
Post a Comment