03 August 2011

Agizo la CCM utata mtupu

Ni kuhusu serikali kushusha bei ya mafuta ya taa
*Wadau wahoji iweje chama kiipinge serikali yake

Gladness Mboma na Stela Aron

SIKU moja baada ya Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuiagiza serikali kutafuta njia za kushusha bei ya mafuta ya taa, Wananchi wa kada mbalimbali wamesema uamuzi huo ni kielelezo kwamba serikali imeparaganyika na inakoelekea ni kubaya.


Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti Dar es Salaam jana, aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu alisema kauli zinazotolewa na serikali na chama, juu ya bei ya mafuta ya taa nchini zinawachanganya Watanzania.

"Nakumbuka awali, Baraza la Mawaziri lilipokaa lilijadili kuhusu suala la uchakachuaji wa mafuta, ambapo wote kwa pamoja walikubaliana kwamba ili kudhibiti uchakachuaji bei ya mafuta ya taa ipandishwe.

"Cha kusikitisha leo (jana) katika vyombo vya habari Kamati Kuu ya CCM nayo imezungumzia suala hilo la mafuta na kuitaka serikali kutafuta njia za kususha bei hiyo, kauli hizi zinawachanganya Watanzania, serikali inatoa agizo hili na CCM nayo inatoa agizo, sasa tumsikilize nani?" alihoji.

Prof. Baregu alisema kuwepo kwa taarifa hizo za mchanganyiko inaonesha dhahiri kuwa serikali imechanganyikiwa, kwani si kwa jambo hilo hata katika suala la umeme pia.

Alisema kauli hizo zinatokana na viongozi kutokuwa na maelewano au makubaliano ya agizo lipi litolewe, hivyo suala hili la mafuta kubaki kuwa malumbano ndani ya CCM na serikali.

"Ni kweli bei ya mafuta imekuwa kubwa na kusababisha wananchi wenye kipato cha chini kushindwa kumudu bei ya mafuta, jambo ambalo limekuwa ni hatari na kuleta gumzo kila kukicha nchini," alisema.

Alisema serikali ilitakiwa kuangalia kwanza suala la kodi ya mafuta yanayotozwa kwa wafanyabiashara na pia faida inayopatikana kwa wafanyabiashara ili kuwepo na uwiano.

Kwa mujibu wa Profesa Barefu kodi ya mafuta iko juu jambo ambalo pia linaathiri uchumi wa nchi na kufanya maisha ya Watanzania kuendelea kuwa maskini.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF-Bara), Bw. Julius Mtatiro alisema hali hiyo inaonyesha kuwa CCM sasa imechanganyikiwa kutokana na kudakia mambo ambayo serikali yake ilikwishayatolea maamuzi.

"CCM imechoka kufikiria na ndio maana sasa imechanganyikiwa kutokana na kauli zao za kujichganganya wasipoangalia sasa wanaipeleka nchi vitani," alisema.

Alisema kauli iliyotolewa juzi na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi (NEC), Bw. Nape Nnauye kuwa serikali itafute njia za kushusha bei ya mafuta ya taa ni ya kinafiki kwa kuwa CUF walikwishatoa kauli hiyo katika mkutano na waandishi wa habari mwanzoni mwa mwezi uliopita.

Bw. Mtatiro alisema asilimia 86 ya Watanzania wanategemea mafuta ya taa, wengine umeme, hivyo kitendo cha kupanda kwa gharama ya mafuta kinaweza kupandisha munkari kwa Watanzania na kuanza kuleta vurugu.

"Watanzania wengi wanatumia koroboi ambazo zinatumia mafuta vijijini na mijini, hivyo kupanda kwa bei ya mafuta ya taa ni hatari kwao," alisema.

Hata hivyo, Bw. Mtatiro aliitupia lawama CCM kwa madai ya kwamba inawathamini wafanyabiashara wakubwa ambao ndio wafadhili wao na hivyo kushindwa kuwachukulia hatua.

Naye Waziri Kivuli wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. John Mnyika, alisema Kamati Kuu ya CCM ilipaswa kutoa agizo la kukubaliana na maoni ya Bajeti Mbadala ya Nishati na Madini iliyotolewa na Kambi ya upinzani Julai 15, mwaka huu ambayo ilipendekeza kodi hiyo ifutwe.

Pia alisema CCM ilitakiwa kuiagiza serikali kuwasilisha muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Fedha katika mkutano wa bunge unaoendelea, ili kupunguza gharama za maisha kwa wananchi kwa kuondoa ongezeko kubwa lililofanywa kwenye kodi ya mafuta ya taa na pia kupunguza kodi zaidi kwenye dizeli na petroli.

4 comments:

  1. ndiyo maana tunasema wana CCM wenge ni wanafiki, hasa viongozi. serikali ikifanya jambo zuri wanasema serikali ya CCM imefanya hivi vizuri kutokana na sera nzuri za CCM. Ikifanya vibaya wanaikana, na hawasemi kama ni serikali hiyohiyo ya CCM iliyoboronga.

    ReplyDelete
  2. you need to put the date of publication on the blog posts. Mtu akiona stori hi hatajua imetokea lini.

    ReplyDelete
  3. Serikali ya CCM haiwezi kudhibiti wafanyabiashara, maana wao ndiyo wanakiendesha chama na vigogo wengi ni wafanyabiashara. hakuna chombo madhubuti cha kudhibiti biashara huria, ndiyo maana inaitwa sasa biashara holela. Pia hii imeonyesha weakness kubwa kwa Rais wetu JK, kiwa mwenyekiti wa baraza la mawaziri alipitisha kupandisha, anakuja kwenye chama akiwa mwenyekiti wa chama anapitisha kushusha. Hii kitu imetuchanganya sana sisi wananchi na kuwa na hofu kuhusu serikali yetu imekosa dira na kutotujali.

    ReplyDelete
  4. Watu walipolalamikia mara kwa mara bei za bidhaa mbalimbali pamoja na bidhaa feki waliambiwa sasa tupo kwenye soko huria ama uchumi wa soko!lakini ni mchezo gani huu usiokuwa na `regulations`ikumbukwe ama ieleweke kwamba China uchumi wao unapaa kwa sababu pamoja na mambo mengine hawakuachia mambo yaende shagalabagala tu eti kwa sababu ya soko huria hii ndiyo athari ya ku copy na kupaste mambo bila kuzingatia mazingira wala historia ya nchi yetu!tusiwe wavivu wa kufikiri!

    ReplyDelete