Na Zahoro Mlanzi
KAMATI ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeirudisha timu ya Shinyanga United kushiriki fainali ya Ligi ya Taifa, baada ya kuridhika na maelezo ya rufani yao waliyokata.
Shinyanga United ambayo ilishika nafasi ya tatu katika Kituo cha Kigoma, sasa itashiriki fainali hizo zinazoanza kesho jijini Tanga.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura, alisema kamati hiyo ilikutana jana chini ya Mwenyekiti wake, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Mstaafu Alfred Tibagana, kusikiliza mashauri mbalimbali yaliyowasilishwa mbele yake.
Alisema timu hiyo ilikata rufani kupinga kuenguliwa kwenye fainali hizo, uamuzi uliofanywa na Kamati ya Mashindano ya TFF, baada ya klabu hiyo kutozingatia maelekezo ya TFF kuhusu usajili wa wachezaji wake.
Alisema ilipinga kuenguliwa ikieleza kuwa, haikupata taarifa yoyote ya maandishi kutoka TFF ikiwazuia kuwatumia wachezaji ambao usajili wao ulikuwa na matatizo na pia usajili wao ulifanywa na TFF.
"Kutokana na hilo ni kwamba, taarifa waliyopewa haikuwa ya kimaandishi, ndio maana kamati ikaona iwarudishe katika mashindano kwa hoja hiyo," alifafanua Wambura.
Awali, nafasi ya Shinyanga United ilikuwa imepewa timu ya Rumanyika SC ya mkoani Kagera ambayo ilikuwa imeshika nafasi ya nne katika kituo hicho kilichokuwa na timu tano.
No comments:
Post a Comment