03 August 2011

Sendeka amkaba koo Magufuli

Na Godfrey Ismaely

Dodoma

MBUNGE wa Simanjiro, Bw. Christopher Ole Sendeka amemkaba koo Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli kwa alichosema ni upandeleo katika ujenzi wa barabara, na hivyo kuitabiria serikali kuanguka kwa kufanya kazi 'kana kwamba ndiyo mwisho ke'.


Hayo yalijitokeza juzi jioni baada ya mbunge huyo kuomba Muongozo wa Spika kutaka ufafanuzi juu ya sababu zilizochangia, hotuba ya Waziri wa Dkt. Magufuli kuonekana ya kero na hata ya kibaguzi kwa upande wa barabara.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, ...nimeisoma hotuba hii nimeona namna ambavyo imegawanyika kibaguzi siwezi kuvumilia kuona maeneo yetu yakiwa yametekelezwa huku barabara ambazo viongozi wanaotoa maamuzi serikalini zikiwa kila mwaka zinapewa kipaumbele.

“Serikali ya namna gani hii inafanya kazi kibaguzi namna hii kama ndiyo inaelekea katika kifo chake, mbona barabara zetu  ambazo sisi viongozi wa ngazi za chini zimekuwa hazipewi kipaumbele, hotuba hii inakera, inaumiza, siwezi kuvumilia ninaomba majibu,” alidai Bw. Sendeka.

Bw. Sendeka alisema kuwa kupitia hotuba ya Waziri ukarasa wa 15-16 kuna vielelezo vya kutosha ambavyo vinaonesha namna ambavyo serikali imeonesha upendeleo mkubwa katika barabara ukiwamo Mkoa wa Kilimanjaro.

Mwenyekiti wa kikao alimuomba Bw. Sendeka atulie ili aweze kupatiwa ufafanuzi wa muongozo wake jana, ambapo baadhi ya wabunge wa CCM ambao walipewa nafasi ya kuchangia katika hotuba ya Wizara ya Ujenzi waliamua kumvaa Bw. Sendeka na kumtaka atulize mpira kwa kuwa tangu zamani walikuwa wamepooza makucha yao lakini kwa sasa wameamka.

Miongoni mwa wabunge ambao walichangia na kumvaa Bw. Sendeka, ni Mbunge wa Manyoni Mashariki-CCM, Bw. John Chiligati ambaye wakati akichangia aliutaja muongozo wa bunge huyo ambao aliutoa awali kuwa siyo sahihi.

“Bajeti hii ukitazama imegawanyika vizuri kwa maendeleo ya taifa letu, hivyo nipingane vikali na muongozo uliotolewa jana na ndugu yangu Bw. Ole Sendeka ambao kwa namna moja ama nyingine siyo wa msingi kwa kuona kwamba watu wa kusini mwaka huu wa fedha wamependelewa kwa ujenzi wa barabara,” alisema
Bw. Chiligati.

Kabla Bw. Chiligati hajamaliza kuchangia, Bw. Sendeka alisimama tena na kutaka kutoa taarifa kwa Spika, akisema, "kanuni ya 68 kifungu cha 8, nimelazimika kuomba muongozo huu, kwani nimevumilia kwa muda bila kupata majibu jambo la kushangaza wajumbe watatu waliopita akiwemo Bw. Chiligati ameamua kuukosoa muongozo wangu na kuweka katika hali ya kwamba jana nilitaka kuigawa nchi kimakundi, hivyo ninataka kuonesha namna ambavyo
hotuba ile ilikuwa imekaa kiupendeleo," alisema na kutakiwa na Spika wa bunge Bi. Anne Makinda akae chini kwa kuwa wakati wa kuwasilisha muongozo siyo lazima atoe hotuba.

Akijibu hoja hizo huku akisema serikali ya CCM haitakufa, Waziri Magufuli alisema barabara za mkoa wa manyara anazozungumzia Bw. Ole Sendeka ni za mkoa ambazo zilipandishwa hadhi mwaka juzi, hivyo isingekuwa rahisi kujengwa kwa kiwango cha lami na kuacha barabara iliyopandishwa hadhi tangu mwaka 1961.

Alisema kwa mkoa wa Kilimanjaro ambapo mbunge huyo alilalamikia upendeleo, baadhi ya barabara zinajengwa na halmashauri na nyingine ni ahadi za rais ambayo tayari zilikuwa zimeshaanza kujengwa na isingekuwa busara kuzinyima fedha.

2 comments:

  1. Chonde chonde watekelezaji wa shughuli za maendeleo ya wananchi. Serikali iwe makini sana katika kupangilia maendeleo suala la upendeleo sio mazuri itafikisha nchi pabaya. Mgawanyo uwe sawa kwa sawa isije tufikisha kama Sudan Kusini kwani walianza hivi hivi mwisho wakaomba kujitenga wapate nchi yao. Hapa kwetu upendeleo wa wazi umeshaanza kujionyesha viongozi wanataka maendeleo yaelekezwe wanakotokea. Namna hii hatutafika wote sisi ni wa-TZ hivyo rasilimali ni zetu sote bila kujali kabila, jinsia na u-kanda.
    Viongozi kuweni macho sana na hili litaleta mgawanyiko usio na ulazima kwa nchi yetu.

    ReplyDelete
  2. MAGUFULI UKO JUU KAKA MIMI NAKUSUBIRIA TU UWE RAIS WANGU KAKA MWAKA 2015.

    ReplyDelete